Israel imetegemea fatuwa za Mashekhe wa Saudia kuwaua Wapalestina
Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel linasema linawaua Wapalestina wanaoandamana kwa kutegemea fatuwa ya mashekhe wa Kiwahhabi kutoka Saudi Arabia.
Jana Wapalestina 17 walikufa shahidi baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel waliokuwa wakizuia maandamano ya Siku ya Ardhi katika Ukanda wa Ghaza. Akizungumza Ijumaa, msemaji wa jeshi la utawala haramu wa Israel Avichay Adraee aliashiria fatuwa ya shekhe maarufu wa Saudia Saleh al-Fawzan ambaye alisema maandamano ya hadhara hupelekea Waislamu wawe makafiri. "Mwanazuoni wa Saudia, Sheikh Saleh al-Fawzan, ametoa fatuwa ya kupiga marufuku maandamano na migomo, na kusema tabia kama hiyo inakiuka maadili ya Waislamu na ni sifa ya makafiri," Adraee amesikika akisema katika mkanda wa video.
Fatuwa hiyo ya mwaka 2011 ya Fawzan, ambaye anayatazama maandamano kama aina fulani ya utovu wa nidhamu, ndiyo ambayo pia ilitumiwa na jeshi la Saudia katika kuzima maandamano makubwa ya wakaazi wa mashariki mwa ufalme huo. Msemaji wa jeshi la utawala haramu wa Israel pia aliashiria fatuwa nyingine ya mwanazuoni wa Saudia Sheikh Ibn Uthaymeen ambaye alisema maandamano na migomo ni 'uovu kwa sababu husababisha ghasia'.
Kwa kutegemea fatuwa hizo, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel jana waliwaua Wapalestina wasiopungua 17 na kuwajeruhi mamia ya wengine waliokuwa wakiandamana kwa amani wakidai haki ya kurejea katika ardhi zao zilizoporwa na utawala huo katili.