Hamas yaitaka Arab League iishtaki Israel katika mahakama ya ICC
(last modified Tue, 03 Apr 2018 13:45:53 GMT )
Apr 03, 2018 13:45 UTC
  • Hamas yaitaka Arab League iishtaki Israel katika mahakama ya ICC

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imeitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuwasilisha faili la mauaji yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Mwito huo umetolewa na Ismail Haniyah, Kiongozi wa Hamas katika mazungumzo yake ya simu na Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League na kuongeza kuwa, mbali na kesi hiyo kuwasilishwa ICC, kuna haja ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha kujadili jinai hizo za kutisha za jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Kwa upande wake, Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa  Jumuiya ya Nchi za Kiarabu sanjari na kulaani ukatili huo wa jeshi la Israel dhidi ya Palestina, amesema jumuiya hiyo inafuatilia kwa karibu mauaji hayo yanayofanywa dhidi ya watu wanaofanya maandamano ya amani kwa ajili ya kutetea haki zao za msingi.

Ismail Haniyah, Kiongozi wa Hamas

Wapalestina wasiopungua 18 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,500 wamejeruhiwa na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano hayo yaliyopewa jina la 'Haki ya Kurejea' siku ya Ijumaa.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa tangu tarehe 6 Desemba mwaka 2017 wakati Trump alipoitangaza Quds tukufu kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Wapalestina 52 wameshauwa shahidi kwa kupigwa risasi na Wazayuni na wengine zaidi ya 9,000 wamejeruhiwa.

Wapalestina wakimbeba mmoja wa majeruhi katika mpaka wa Gaza

Tags