Matokeo ya kufunguliwa kituo cha kijeshi cha Uingereza nchini Bahrain
Uingereza imefungua kituo chake cha kwanza cha kudumu cha kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi huko katika Bandari ya Salman nchini Bahrain.
Kituo hicho cha kijeshi kilichopewa jina la Misaada ya Kilojestiki ya Bahrain kilifunguliwa siku ya Alkhamisi kwa kuhudhuriwa na Salman bin Hamad Aal Khalifa, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Bahrain. Manama na London zinafuatilia malengo maalumu katika kuimarisha uhusiano wao wa kijeshi ambao hatimaye utaimarisha nafasi ya kijeshi ya Uingereza kusini mwa Ghuba ya Uajemi. Katika mazingira ya hivi sasa ambapo utawala wa Manama unakabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko ya wananchi, utawala huo unakusudia kutumia askari wa Uingereza kuzima moto wa mapinduzi ya wananchi hao. Kuhusu suala hilo, gazeti la Uingereza la Daily Mail liliandika hivi karibuni kwamba serikali ya London inawapa mafunzo askari jeshi na wa usalama wa Bahrain na wa nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia. Bahrain ambayo ni mwenyeji wa kikosi cha tano cha baharini cha wanamaji wa Marekani imekuwa uwanja wa harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa ukoo wa Aal Khalifa.
Wananchi hao wanapigania uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali ambayo imechaguliwa na wananchi wenyewe, lakini wamekuwa wakikabiliwa na mkono wa chuma wa watawala vibaraka wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo ukandamizaji huo umekuwa ukinyamaziwa kimya na serikali za Magharibi ikiwemo ya Uingereza. Kwa msingi huo, gazeti la nchi hiyo la Independent limeandika kuwa kujengwa kituo kilichotajwa cha kijeshi nchini Bahrain ni zawadi ya watawala wa Manama kwa serikali hiyo ya Magharibi kutokana na kimya chake mbele ya ukandamizaji unaotekelezwa na watawala hao dhid ya raia wa nchi hiyo. Ujenzi wa kituo hicho umegharimu karibu pauni milioni 15 ambazo zimelipwa na utawala wa Manama. Licha ya hayo, serikali ya London bado ina matarajio mengine kutoka kwa utawala huo. Uingereza bado haijasahau kipindi cha ukoloni wake katika nchi za Ghuba ya Uajemi na kwa hivyo inataka kujiimarisha tena nchini Bahrain.
Uingereza kama zilivyo nchi nyingine za Magharibi zinazotengeneza silaha, inataka kuziuzia nchi za Ghuba ya Uajemi silaha hizo na kwa hivyo inatafuta kisingizio kizuri cha usalama ili ijiandalie fursa ya kuweza kujiimarisha kijeshi katika nchi za Kiarabu za kusini mwa Ghuba ya Uajemi. Kabla ya kuondoka katika eneo hilo katika muongo wa 1970, Uingereza ilikuwa nchi muhimu zaidi ya Magharibi iliyokuwa na ushawishi katika eneo hilo. Nchi hiyo ilikuwa na nafasi muhimu katika kubuni mfumo wa hivi sasa wa kisiasa wa nchi za Mashariki ya Kati na imekuwa ikiendela kuzishawishi nchi za Kiarabu ziitegemee katika karibu ikila jambo ili kwa njia hiyo iweze kulinda maslahi yake. Bahrain ni moja ya nchi zilizo na umuhimu mkubwa kwa Uingereza na serikali ya London imeendelea kulinda maslahi yake nchini humo kupitia utawala kibaraka wa Aal Khalifa.
Nchi hiyo ya Magharibi imeendelea kujidhaminia maslahi yake ya kiuchumi kwa kulinda maslahi ya kiusalama ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambapo Bahrain ni mwanachama. Kwa maelezo hayo, Uingereza inataka kuhuisha nafasi yake ya kikoloni katika eneo na ni wazi kuwa nafasi hiyo imeingia katika awamu mpya kwa kuzingatia mashindano ya kupora mali na utajiri wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, yanayoendelea kati ya Uingereza na Marekani inayotawaliwa na Donald Trump ambaye ameapa kuendelea kuzikamua nchi hizo za Kiarabu zinazotawaliwa na watawala vibaraka wasiojali maslahi ya wananchi wao.