Hamas yajibu vitisho vya Israel, yasema maandamano yataendelea
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema maandamano makubwa ya amani yataendelea hadi pale mzingiro wa kibaguzi katika Ukanda wa Gaza utakapoondolewa.
Hayo yalisemwa na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas hapo jana akihutubia mkusanyiko wa waandamanaji katika mpaka wa Gaza.
Amefafanua kuwa, "Tutarejea katika Palestina yetu, katika vijiji vyetu na katika mji wetu mtakatifu wa Quds. Ingawaje ni wiki ya pili tu sasa tunafanya maandamano haya ya amani, lakini yamepata mafanikio makubwa. Huu ni mwanzo tu."
Hapo juzi gazeti la Kizayuni la Haaretz lilinukuu duru za kijeshi za Israel zikisema kuwa, vikosi katili vya utawala huo haramu vimejiweka tayari kuishambulia Hamas, iwapo Wapalestina wataendelea kufanya maandamano.
Wapalestina zaidi ya 30 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,900 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano ya Siku ya Ardhi yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yaliyoanza huko Gaza Ijumaa ya Machi 30.