Ismail Haniya: Waliomuua mwanasayansi wa Kipalestina watalipa gharamu kubwa
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema wahusika wa mauaji ya Fadi al Batsh, mwanachama msomi wa harakati hiyo, watalipa gharama kubwa kwa kumuua mwanasayansi huyo nchini Malaysia.
Katika mahojiano na Kituo cha Habari cha Palestina, Ismail Haniya amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unabeba dhima ya mauaji ya mhadhiri na mhandisi huyo wa masuala ya umeme na unapaswa kujiandaa kwa jibu kali.
Haniya amesisitiza kuwa, Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) limehusika na mauaji ya mwanasayansi huyo wa Kipalestina aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu huko Kuala Lumpur, Malaysia.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina amebainisha kuwa, al Batsh ameacha rekodi na utendaji unaong'ara katika elimu ya sayansi, imani na kuhudumia malengo na wananchi wa Palestina na vilevile Umma wa Kiislamu na wanadamu wote.
Fadi Muhammad al Batsh mwanasayansi mtajika wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 35 ambaye aliwahi kupokea tuzo bora ya utafiti katika Ulimwengu wa Kiarabu aliuawa shahidi Jumamosi wakati akitoja katika Swala ya alfajiri karibu na nyumbani kwake mtaa wa Idaman Puteri, viungani mwa Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia.
Kwa mujibu wa Mazlan Lazim, Kamanda Mkuu wa Polisi mjini Kuala Lumpur, msomi huyo wa Kipalestina aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wawili waliokuwa juu ya pikipiki, na kwamba kamera za CCTV zinaonyesha kuwa makatili hao walikuwa katika eneo la tukio dakika 20 wakimsubiri mwanasayansi huyo wa Kipalestina.