"Maandamano ya Haki ya Kurejea" nembo endelevu ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43794-maandamano_ya_haki_ya_kurejea_nembo_endelevu_ya_wapalestina
Yahya Sinwar Mwanachama wa Ngazi za Juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesisitiza kuhusu kuendelea "Maandamano ya Haki ya Kurejea" na kusema: "Maandamano makubwa ya Wapalestina katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel mwaka 1948 ni ishara ya kufungamana na haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Apr 29, 2018 03:01 UTC

Yahya Sinwar Mwanachama wa Ngazi za Juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesisitiza kuhusu kuendelea "Maandamano ya Haki ya Kurejea" na kusema: "Maandamano makubwa ya Wapalestina katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel mwaka 1948 ni ishara ya kufungamana na haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao.

Siku ya Ijumaa maelfu ya Wapalestina waliandamana katika maeneo ya mpakani ya Ukanda wa  Ghaza katika Ijumaa ya tano ya maandamano makubwa ya 'Haki ya Kurejea". Kauli mbiu ya maandamano ya Ijumaa hii ilikuwa ni 'Ijumaa ya Vijana Wanamapinduzi." Lengo la kufanyika maandamano hayo ni kusisitiza haki ya kurejea Wapalestina katika ardhi zao ambazo ziliporwa na Wazayuni.

Kilele cha maandamano hayo kitakuwa ni katikati ya Mwezi Mei wakati ambao Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza atauhamisha ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv hadi mji wa Quds Tukufu (Jerusalem). Tokea Ijumaa Machi 30 wakati maandamano ya 'Haki ya Kurejea' yalipoanza hadi sasa, Wapalestina wapatao 49 wamefyatuliwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huku wengine zaidi ya 6000 wakijeruhiwa.  Maandamano hayo makubwa ya Wapalestina yamekuwa ni pigo kubwa kwa rais wa Marekani na baadhi ya waitifaki wake wahaini katika nchi za Kiarabu ambao wanataka kadhia ya Palestina imalizike kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Manuel Musallam, Kasisi Mkatoliki huko Palestina katika mahojiano na mtandao wa habari wa 'Filistin Al Youm' ametaka utangazwe uasi wa kiraia kama mojawapo ya mbinu za muqawama au mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israeli hadi pale Wapalestina watakapofikia takwa lao la kuikomboa nchi yao inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni. Amesema uasi wa Kiraia ni aina ya mapambano ambayo yanatuma ujumbe wa kistaarabu kwa wanadamu wote duniani na kwamba uasi kama huu umekuwa na taathira katika vipindi mbali mbali vya historia katika mapambano dhidi ya madhalimu.

Wapalestina katika 'Maandamano ya Kurejea' 

"Maandamano ya Kurejea" ni mfano wa hivi karibini kabisa wa jitihada za Wapalestina za kupigania haki zao walizopokonywa na hakuna shaka katika hali ya hivi sasa katika eneo, mbinu hii inatazamiwa kuwa na mafanikio ya kipekee.

Kunahitajika uchunguzi zaidi kubaini ni kwa nini kumeibuka wimbi jipya la mwamko miongoni mwa Wapalestina. Pamoja na hayo katika miezi ya hivi karibuni tumeshuhudia kusambaratika fitina ya wakufurishaji na kuhuishwa tena kadhia ya Palestina kieneo na kimataifa.

Moja ya malengo makuu ya kuibuka, kuenea na kupata nguvu harakati za magaidi wakufurishaji katika eneo la Asia Magharibi na kuzishughulisha nchi za Kiislamu na vita vya ndani ni kujaribu kuwafanya Waislamu wasahau kadhia nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu, yaani kadhia ya Palestina.

Wakati nchi za Kiislamu na Kiarabu zinapotumbukia katika lindi la migogoro ya ndani, ukosefu wa usalama na ugaidi, hata kama zinataka, haziwezi kuwa nguzo imara ya kuunga mkono Wapalestina katika jitihada zao za ukombozi hasa kwa kuzingatia kuwa nchi zilizo katika mstari wa mbele wa kutetea Wapalestina kama vile Iraq na Syria zimelengwa na kutumbukizwa katika vita.

Mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel

Kwa msingi huo kuondolewa fitina ya magaidi wakufurishaji ni fursa nyingine kwa ajili ya kuangazia kadhia ya Palestina na kaundaa mazingira ya kutenga mrengo wa baadhi ya madola ya Kiarabu na Magharibi ambayo yanataka kuwepo uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na hatimaye kuwasaliti Wapalestina. Katika hali kama hii mwamko wa taifa la Palestina unachukua sura mpya kila siku na unazidi kuenea ambapo ushindi wa mrengo wa muqawama katika vita na fitina kubwa ya wakufurishaji ni jambo ambalo limeipa uhai mpya kadhia ya Palestina. Hali hii imethibitisha tena kuwa, kusimama kidete mbele ya madhalimu na kutetea haki ndio njia pekee ya kutatua kadhia ya Palestina. Matukio ya hivi sasa Palestina yanaonyesha kuwa, "Maandamano ya Kurejea" ni sehemu ya muqawama au mapambano ya taifa la Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 'Maandamano ya Kujrea" si harakati ya muda mfupi bali ni harakati endelevu na itadumu hadi pale Wapalestina watakapofikia na kufanikisha malengo yao yote matukufu.