HAMAS: Maandamano ya Wapalestina katika mpaka wa Gaza yataendelea
(last modified Tue, 15 May 2018 08:02:29 GMT )
May 15, 2018 08:02 UTC
  • HAMAS: Maandamano ya Wapalestina katika mpaka wa Gaza yataendelea

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa maandamano ya amani ya Wapalestina katika mpaka wa Ukanda wa Gaza ya kupinga ubalozi wa Marekani Tel Aviv kuhamishiwa Baitul Muqaddas yataendelea.

Khalil Al-Hayyah, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa serikali ya Marekani inabeba dhima ya matokeo yote hasi yatakayosababishwa na hatua yake ya kuuhamishia Quds ubalozi wake wa Tel Aviv na kuongeza kuwa hatua hiyo ni jinai ya kuaibisha na kufedhehesha na kwamba kimya cha Hamas na brigedi za Izzuddin Al Qassam, tawi la kijeshi la harakati hiyo kwa jinai zinazofanywa na Israel hakitoendelea kwa muda mrefu.

Khalid Al-Batsh, mkuu wa jopo kuu la uongozaji maandamano ya Haki ya Kurejea naye pia ameeleza katika mkutano huo na waandishi wa habari kuwa, maandamano ya umma na ya amani ya Wapalestina dhidi ya hatua ya Marekani yangali yanaendelea na kwamba Wapalestina hawatonyamazia kimya na kuangalia tu jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wapalestina wakiandamana katika mpaka wa Gaza

Al-Batsh aidha amesema, leo ni siku ya maombolezo katika ardhi zote za Palestina na ya mgomo katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wakati huohuo Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa kutokana na kuongeza idadi ya majeruhi, Wapalestina wanatakiwa wafike mahospitalini kwa ajili ya kuchangia damu.../

Tags