EU yatakiwa kususia bidhaa zinazozalishwa na Wazayuni
Umoja wa Ulaya umetakiwa kususia bidhaa zinazozalishwa na utawala wa kizayuni wa Israel.
Wito huo umetolewa na Rami Hamdallah, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alipokutana na kufanya mazungumzo na Chistian Berger, Mkurugenzi wa Masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Masuala ya Nje ya Ulaya EEAS, mjini Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan jana Jumatatu. Hamdallah amezitaka nchi zote za Ulaya kusimamisha uagizaji wa bidhaa zinazozalishwa na utawala haramu wa Israel ndani ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Kadhalika Waziri Mkuu wa Palestina amezitaka nchi za Umoja wa Ulaya kulitambua rasmi taifa huru la Palestina na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia wa moja kwa moja.
Aidha Rami Hamdallah, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amezitaka nchi 28 wanachama wa EU kuunga mkono kwa hali na mali wazo la kufanyika kuongamano la kimataifa la kutafuta amani ya kudumu Mashariki ya Kati.
Waziri Mkuu wa Palestina ameutumia mkutano huo pia kumweleza afisa huyo wa EU kuhusu hali mbaya ya kibinadamu wanayopitia Wapalestina kutokana na mzingiro haramu wa Tel Aviv dhidi yao.
Zaidi ya raia 200 wa Palestina wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel tangu kuanza kwa mapambano ya Intifadha ya Quds mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana. Maelfu ya wengine wamejeruhiwa na wengine kuzuiliwa chini ya mazingira ya kuogofya katika jela za utawala huo haramu.