Magaidi wakufurishaji wabomoa makaburi katika kusaka mali na dhahabu Afrin, Syria
Magaidi wakufurishaji nchini Syria wamevamia makaburi ya shakhsia wa kidini na wanaoheshimiwa wa mji wa Afrin katika kusaka mali na dhahabu ndani ya makaburi hayo.
Gazeti la al-Watan la nchini Syria limevinukuu vyanzo vya habari vya mji wa Afrin kwamba, tukio hilo lilianza baada ya magaidi hao wenye kufuata theolojia ya Kiwahabi kupata habari kwamba baadhi ya wakazi wa mji huo walifukia mali na dhahabu zao katika maeneo ya makaburini kwa lengo la kuzuia zisiporwe na magaidi.
Kufuatia hali hiyo magaidi hao wamevamia maeneo yote ya makaburi yakiwemo pia makaburi ya shakhsia wakubwa wa kidini na kuyavunja katika kutafuta mali na dhahabu. Aidha duru za habari zimefafanua kuwa hata kaburi la Sheikh Zaid lililopo eneo la al-Zaidiyah mjini Afrin na ambalo kwa miaka mingi limekuwa likiheshimiwa na Waislamu wa Kikurdi wa mji huo, lilikuwa ni kaburi la mwisho kuharibiwa katika kutafuta mali na dhahabu. Kadhalika magaidi hao wameharibu athari za zamani za mji wa Afrin na mabaki ya hekalu la Ain Dara lenye miaka elfu 10 katika mji huo.
Operesheni za kijeshi za jeshi la Uturuki katika eneo la Afrin chini ya anwani ya 'Tawi wa Mzaituni' zilianza tarehe 20 Januari mwaka 2018 ambapo katika operesheni hizo mamia ya raia wa eneo tajwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Aidha operesheni hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa makazi ya raia na kuwalazimu maelfu ya raia kuwa wakimbizi.