Wito wa maulamaa wa Afghanistan wa kukomeshwa vita nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45464-wito_wa_maulamaa_wa_afghanistan_wa_kukomeshwa_vita_nchini_humo
Mashekhe na maulamaa elfu tatu wa Afghanistan wametoa wito wa kukomeshwa vita na machafuko nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2018 22:01 UTC
  • Wito wa maulamaa wa Afghanistan wa kukomeshwa vita nchini humo

Mashekhe na maulamaa elfu tatu wa Afghanistan wametoa wito wa kukomeshwa vita na machafuko nchini humo.

Maulamaa hao wametoa wito huo katika kongamano maalumu lililofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul. Washiriki wa kongamano hilo wameyataka makundi yanayoipinga serikali yakomeshe vita na kutangaza usitishaji mapigano kwa heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Washiriki wa kongamano la Kabul wameyataka makundi yanayoshupalia vita likiwemo la Taliban yakomeshe vita haraka iwezekanavyo, "kuweka chini silaha zao" na kufikia suluhu.

Katika kongamano lao hilo, maulamaa wa Afghanistan vilevile wamelitaka kundi la Taliban lifanye mazungumzo na serikali ili kufikia suluhu na kuhitimisha vita na mauaji nchini humo.

Maulamaa hao aidha wamesisitiza kwamba asilimia 99 ya Waafghani ni Waislamu na kwamba vita katika jamii kama hiyo vinakinzana na sharia za Kiislamu.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Taiban

Kwa mujibu wa mashekhe na maulamaa wa Afghanistan, raia Waislamu wa nchi hiyo ndio pekee waliokuwa mhanga wa vita vya miongo mitatu vilivyotokea nchini humo; na kwa sababu hiyo vita hivyo ni haramu. 

Hii si mara ya kwanza kwa maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu nchini Afghanistan kutoa wito wa kukomeshwa vita kwa makundi yanayobeba silaha yanayoipinga serikali ya nchi hiyo.

Katika miaka ya karibuni na katika vikao mbalimbali walivyofanya ndani na nje ya nchi, maulamaa wa Afghanistan wamesisitiza kuwa vita na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo ni haramu na wamejaribu kufanya juhudi za kuyashawishi makundi na mirengo hasimu kukomesha mapigano na machafuko hayo.

Ndani ya jamii ya Afghanistan kuna mtazamo kwamba shakhsia na wanazuoni wa Kiislamu wana ushawishi mkubwa kwa Waislamu wa nchi hiyo; na kwa hivyo wanaweza kutumia ushawishi wao kusaidia kurejesha uthabiti na utulivu nchini humo.

Maulamaa wa Afghanistan

Na hasa kwa kuzingatia kwamba makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Afghanistan likiwemo la Taliban, ambalo idiolojia yake inazitolea tafsiri isiyo sahihi hukumu za dini tukufu ya Uislamu, linaitakidi kuwa, vita linavyopigana ni aina mojawapo ya Jihadi, jambo ambalo linakinzana kikamilifu na misingi ya dini hiyo tukufu inayoshajiisha suluhu na amani.

Ni kwa sababu hiyo, maulamaa wa Afghanistan wamelipinga dai hilo la Taliban na kutangaza kuwa hujuma za kigaidi na mashambulio ya kuripua mabomu yanayofanywa na kundi hilo kwa jina la jihadi ni haramu kisharia na wala hayana uhusiano wowote na misingi ya hukumu za dini tukufu ya Uislamu.

Kwa kuzingatia kuwa makundi yenye misimamo ya kufurutu ada kama lile la Taliban linadai kwamba mashambulio na hujuma zake za umwagaji damu zinazokinzana na misingi ya utu linazifanya kwa msingi wa dini, kutojali kwao fatua za maulamaa wa Afghanistan za kuharamisha vita vinavyopiganwa nchini humo na badala yake kuendeleza machafuko na mauaji ni ithibati kamili kwamba kundi la Taliban halifuati misingi ya wazi ya dini ya Uislamu inayotilia mkazo suluhu na upendo.

Moulawi Ataullah Ludin, mmoja wa maulamaa wa Afghanistan anasema: "Vita nchini Afghanistan ni kwa madhara ya Uislamu na Waislamu; na hapa ndipo vilipotufikisha. Kwa bahati mbaya, kutokana na makundi ya kigaidi katika eneo kuitumia vibaya tafsiri ya Uislamu, Afghanistan ingali inateketea kwenye moto wa vita huku misikiti, maskuli na mahospitali yakiwa yangali yanashambuliwa, raia wanaendelea kuuawa masokoni na hata hujuma za miripuko ya mabomu zinawaandama watu wanaohudhuria mikusanyiko ya maziko."

Kizazi cha ukoo na utawala wa Aal Saud unaoeneza Uwahabi na ugaidi Afghanistan

Tab'an mbali na madai potofu ya Taliban ya kufuata Uislamu, tukumbuke pia kwamba kuendelea machafuko na umwagaji damu unaofanywa na kundi hilo kunachangiwa pia na nafasi ya baadhi ya nchi kama Saudi Arabia inayoeneza fikra za Uwahabi na vita katika jamii za Kiislamu.

Hussein Naseri, mbunge wa Afghanistan analizungumzia suala hilo kwa kusema: Viongozi wa Saudi Arabia wanalipatia kundi la Taliban mamilioni ya dola kwa malengo kadhaa, yakiwemo ya kuanzisha vita vya kimadhehebu na mivutano ya kikabila katika nchi za Afghanistan na Pakistan.

Katika mazingira kama hayo inaonesha kuwa maadamu Saudi Arabia inaendelea kulifadhili kifedha kundi la Taliban huku maulamaa wa Kiwahabi nao wakiendelea kueneza na kukoleza moto wa itikadi yao inayochochea ukatili na mauaji, Taliban na makundi mengine ya kigaidi yatazidi kuhamasishika kufanya mauaji na umwagaji damu; na ni baidi kwamba juhudi zinazofanywa kukomesha vita nchini Afghanistan zitaweza kuwa na tija inayotarajiwa.../