Kufichuliwa njama ya Marekani ya kuingiza tena magaidi nchini Iraq
Matukio ya mwaka mmoja uliopita nchini Iraq ambapo magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh wamesambaratishwa na kutumiliwa kikamilifu kutoka maeneo yote waliyokuwa wameyateka kufuatia jitihada za jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi, yameiandaa Iraq kuingia duru mpya ya baada ya Daesh na kuandaa mazingira ya uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi uliopita.
Matokeo ya uchaguzi wa Iraq yanaonyesha kuwa, Wairaqi wanachukizwa na kuwepo wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi yao. Matokeo ya uchaguzi huo yanabainisha kuwa Wairaqi wamepiga kura kwa ajili ya uhuru, usalama na kulindwa mipaka ya nchi hiyo na La kwa uvamizi wa Marekani. Ni wazi kuwa subira ya watu wa Iraq imefika ukingoni kuhusu uingiliaji kijeshi wa Marekani katika nchi hiyo kwa visingizio mbali mbali.
Sayyed Hamid Husseini' Mkuu wa Jumuiya ya Radio na Televisheni za Iraq anasema: "Karibu wajumbe 200 waliochaguliwa katika bunge la Iraq hivi karibuni ni kutoka mirengo ya muqawama ambayo inapinga uvamizi na ubeberu wa Marekani. Ameongeza kuwa magaidi wa ISIS wameangamizwa kikamilifu Iraq na kubaini kuwa: "Ushindi wa mirengo ya muqawama Iraq ni sawa na ushindi wa Hizbullah nchini Lebanon na jambo hilo limewakasirisha mabeberu wa Magharibi katika eneo na vibaraka wao katika nchi za Kiarabu. Ameendelea kusema kuwa: Katika uchaguzi wa mwaka 2014, viti 183 katika bunge la Iraq vilichukuliwa na mrengo wa muqawama na katika mwaka 2018 idadi hiyo ya wabunge wanaopinga Marekani kikamilifu imeongezeka na kufika 200 kati ya viti vyote 329 katika bunge hilo.
Ni wazi kuwa njama ambazo Markeani imekuwa ikipanga nchini Iraq kama vile kuchochea magaidi na kuunga mkono makundi yanayotaka kujitenga zimegonga mwamba.
Lakini pamoja na kufeli huko Marekani ingali inapanga njama mpya na sasa kuna taarifa kuwa, Washington inayafadhili makundi ya magaidi wakufurishaji ili waanzishe tena vurugu huko Iraq. Duru zinadokeza kuwa Marekani inataka kuwaingiza Iraq magaidi ambao wamepata pigo hivi karibuni nchini Syria.
Matukio ya eneo la Asia Magharibi katika miongo ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa, kila nchi ambayo Marekani inaiingilia moja kwa moja kijeshi, huharibiwa vibya na makundi hatari ya kigaidi kuibuka katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na Marekani.
Harakati ya al-Nujaba ya Iraq imefichua kuhusu njama mpya ya Marekani kuondoa wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Wapiganaji wa Kujitoela , Hashd al Shaabi, kutoka katika mpaka wa Iraq na Syria ili kuandaa mazingira ya kuingia magaidi Iraq.
Hakuna shaka kuwa, ili kuhalalisha kuendelea kubakia Iraq, Marekani inalenga kuibua makundi ya kigaidi nchini humo. Wakuu wa Marekani wanataka kubakia Iraq kwa msingi wa eti kupambana na ISIS na hivyo wanafanya juu chini kuhakikisha kuwa ugaidi haumaliziki Iraq ili kupata fursa ya kuendeleza mipango yake ya kibeberu dhidi ya nchi hiyo kubwa ya Kiarabu yenye umuhimu wa kistratijia na utajiri wa mafuta.
Wananchi wa Iraq wanafahamu na kudiriki vyema njama hizo haribifu za Marekani na ni kwa msingi huo ndio wakasisitiza kuwa moja ya matakwa yao makuu kwa viongozi wa nchi hiyo ni kuondoka kikamilifu wanajeshi vamizi wa Marekani nchini humo.