HAMAS yapongeza azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu wananchi wa Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imepongeza azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifra la kuwahami na kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, leo Alkhamisi harakati ya HAMAS imetoa tamko na kulipongeza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kupiga ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kupinga pendekezo la Marekani la kutaka kulaaniwa harakati ya HAMAS. Harakati hiyo imesema, hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ni ushindi mkubwa kwa taifa la Palestina na ni kuzidi kutengwa Marekani kimataifa.
Imesisitiza kuwa, Marekani inafanya njama za kuficha jinai za kila leo za utawala wa Kizayuni wa Israel na kutafuta njia za kila namna kuzihalalisha.
Taarifa hiyo ya HAMAS pia imesema, azimio hilo la Umoja wa Mataifa litaitia nguvu misimamo rasmi na ya kimataifa ya Wapalestina na hii ni katika hali ambayo, kwenye kipindi chote hiki cha miongo kadhaa iliyopita, Wapalestina wamekuwa wakiwaonesha walimwengu ushahidi wa kila namna kuhusu dhati ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai zake zisizo na kifani dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Taarifa hiyo ya HAMAS imeongeza kuwa, uungaji mkono wa kweli kwa wananchi madhlumu wa Palestina ni kulisaidia taifa hilo kuiangamiza Israel na kupandishwa kizimbani viongozi watenda jinai wa utawala huo dhalimu .
Jana Jumatano tarehe 13 Juni, 2018, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipashisha azimio la kuilaani Israel kwa kuwaua kiholela wananchi wa Palestina. Azimio hilo limepasishwa kwa kura 120 za ndio.