Bahrain yawakaribisha rasmi wajumbe wa utawala wa Kizayuni wa Israel
Afisa mmoja wa Bahrain ametangaza habari ya kushiriki ujumbe mmoja rasmi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa kiutamaduni nchini Bahrain.
Hayo ni kwa mujibu wa televisheni ya Rusia al Yaum ambayo imemnukuu Munir Bushnaqi, mmoja wa maafisa wa Taasisi ya Utamaduni na Athari za Kale ya Bahrain akisema kuwa, ujumbe mmoja rasmi wa Israel utashiriki katika mkutano wa kiutamaduni wa kimataifa nchini Bahrain.
Amesema, mkutano huo wa kimataifa umepangwa kufanyika tarehe 24 mwezi huu wa Juni na utaendelea hadi tarene 4 Julai nchini Bahrain chini ya usimamizi wa Shirika Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Kwa mujibu wa afisa huyo wa Bahrain, idadi ya watu walioalikwa kushiriki katika mkutano huo ni zaidi ya elfu mbili kutoka mabara tofauti ya dunia.
Suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel ambao unafanya jinai za kutisha dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, ni katika ajenda kuu ya baadhi ya nchi za Kiarabu na zimeongeza kasi yake baada ya kuingia madarakani mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud mwezi Januari 2015.
Ingawa uhusiano baina ya baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na utawala wa Kizayuni ulikuwepo kabla ya hapo, lakini haukuwa wa wazi wazi kama inavyoshuhudiwa hivi sasa baada ya kuchukua madaraka Salman bin Abdulaziz huko Saudi Arabia.