Qatar yataka Saudia na Imarati zitimuliwe Baraza la Haki za Binaadamu
Baada ya kupita mwaka mmoja tangu kukatwa mahusiano ya nchi za Kiarabu na Qatar na kadhalika kuiwekea vikwazo na mzingiro wa kila upande nchi hiyo, serikali ya Doha imetaka uanachama wa Saudia na Imarati katika Baraza la Haki za Binaadamu usimamishwe.
Hayo yamesemwa na Dr. Ali bin Smaikh Al Marri, mkuu wa kamisheni ya kitaifa ya haki za binaadamu nchini Qatar katika kikao na waandishi wa habari katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswis ambapo pamoja na mambo mengine amelitaka baraza la haki za binaadamu la umoja huo sambamba na kuchukua hatua za kukabiliana na nchi zinazoizingira Qatar na pia kufuatilia ripoti za Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu, Zeid Raad Al Hussein dhidi ya Saudia na Imarati na kisha kusimamisha uanachama wa nchi hizo katika baraza hilo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Qatar, pendekezo la kusimamishwa uachama wa nchi hizo katika baraza hilo linatokana na ukiukaji wa wazi na ulioratibiwa wa haki za binaadamu dhidi ya raia wa Qatar unaofanywa na serikali za Riyadh na Abu Dhabi na kwa msingi wa kipengee cha nane cha azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililounda Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa.
Dr Ali bin Smaikh Al Marri ameashiria udharura wa hatua ya serikali ya Doha katika Baraza la Usalama kwa ajili ya kuwekwa wazi hatua zisizo za kisheria za nchi za Kiarabu zinazoizingira Qatar yaani Saudia, Bahrain, Imarati na Misri na kuongeza kuwa, baadhi ya hatua hizo zinahesabika kuwa za jinai za kivita na kiuchumi na zinazolenga kuwaadhibu wananchi wa Qatar. Nchi hizo za Kiarabu zilitangaza kukata uhusiano wao na serikali ya Doha tarehe tano Juni mwaka jana baada ya nchi hiyo kukataa kuwa chini ya uongozi wa Saudia.