Malaysia yasimamisha ushirikiano wa kijeshi na Saudi Arabia
Waziri wa Ulinzi wa Malaysia ametangaza kuwa, nchi hiyo imesimamisha ushirikiano wake wa kijeshi na Saudi Arabia.
Mohamad Sabu amesema kuwa, nchi hiyo inaondoa askari wake katika muungano unaoongozwa na Saudia katika vita vya Yemen na kuongeza kuwa: Tokeo sasa Malaysia haitashiriki katika vita nchini Yemen na hivi karibuni itapanga jedwali la jinsi ya kuwaondoa askari wake katika muungano wa vita wa Saudia na kuwarejesha nyumbani.
Ushindi wa "Muungano wa Matumaini" unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Malaysia, Mahathir Muhammad katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo umetoa kipigo cha nguvu kwa Saudi Arabia. Waziri Mkuu anayeondoka wa Malaysia, Najib Tun Razak alikuwa na uhusiano mkubwa na Saudia na anatuhumiwa kufanya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma katika ushirikiano wake na serikali ya Riyadh.

Duru za kisiasa zinasema kuwa, kuondoka kwa Malaysia katika muungano wa vita vya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen ni pigo jingine kubwa kwa utawala wa kifalme wa Riyadh. Suala hili tunaweza kulijadili katika pande mbili. Kwanza ni kwamba, muungano wa vita wa Saudi Arabia huko Yemen umefeli na kushindwa, na wananchi wa Yemen na makundi ya mapambano sasa yanaitumbukiza Riyadh katika kinamasi cha Yemen. Pili ni kuwa, kurejea madarakani kwa Mahathir Muhammad huko Malaysia kumebadili mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo kuhusu masuala na matukio ya Ulimwengu wa Kiislamu na sasa Kuala Lumpur inayaunga mkono makundi na harakati za wananchi zinazopambana na wavamizi huko Palestina na Yemen.
Ukweli ni kwamba msimamo huo wa serikali ya sasa ya Malaysia wa kupinga siasa na sera za Saudia huko Yemen ni pigo kubwa na la aina yake kwa Riyadh, hasa kwa kutilia maanani misaada na uungaji mkono wa hali na mali wa Saudi Arabia kwa makundi ya kigaidi kama Daesh na hatua ya hivi karibuni ya mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman ya kujikurubisha zaidi kwa utawala haramu wa Israel.
Mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya nchi za Kiarabu Abdullah al Tamimi anasema: Japokuwa Najib Tun Razak ameondoka madarakani nchini Malaysia lakini kutokana na kwamba, kuna uwezekano akapandishwa kizimbani kwa tuhuma za ufisadi, Saudi Arabia ina wasiwasi wa kupatwa na wimbi la kushindwa kwa muitifaki wake huyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wanamfalme wa Saudi Arabia walishirikiana na Tun Razak katika wizi na uporaji mkubwa wa fedha za umma za Wamalaysia."

Wakati huo huo mabadiliko ya uongozi nchini Malaysia yameifanya Saudi Arabia na mawahabi wapoteze moja ya vituo vyao muhimu katika eneo la kusini mashariki mwa Asia. Uhusiano mkubwa sana uliokuwepo baina ya serikali iliyoondoka madarakani ya Malaysia na watawala wa Saudi Arabia ulitayarisha mazingira ya kuimarishwa na kupanuliwa satua na ushawishi wa mawahabi nchini Malaysia, na duru za kidini nchini humo zimekuwa zikitahadharisha kuhusu athari mbaya na hatari za jambo hilo ikiwa ni pamoja na kupanuka na kuenea kwa makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali nchini humo.
Marina Mahathir ambaye ni mtaalamu wa msuala ya siasa na binti wa waziri mkuu wa zamani wa Malaysia, Mahathir Muhammad anasema: "Kutokana na ushawishi na satua ya Saudi Arabia, Malaysia ilikuwa imeanza kuelekea katika upande wa misimamo ya kufurutu mipaka, na mabadiliko ya mavazi na kuenea utumiaji wa mavazi ya Kiarabu nchini ilikuwa alama na ishara ya kuenea misimamo mikali. Si hayo tu bali baadhi ya wanasiasa walitoa wito wa kutekelezwa sheria kama za Saudi Arabia nchini Malaysia", mwisho wa kunukuu.

Alaa kulli hal, watu wa Malaysia hususan wanawake wa nchi hiyo wameelimika na wanaelewa vyema malengo ya Saudi Arabia ya kutaka kueneza misimamo mikali na itikadi za kufurutu ada za kiwahabi nchini kwao. Wamalaysia wameonesha utambuzi na maarifa yao kwa kuupigia kura muungano wa Mahathir Muhammad na kutoa kipigo kikali kwa aliyekuwa waziri mkuu, Tun Razak. Wamalaysia pia wameonesha kuwa, kamwe hawatairuhusu Saudi Arabia kuipisha magoti nchi yao au kuburutwa na utawala wa kifalme wa Riyadh kwa kutumia nguvu ya dola za Kimarekani na fedha za mafuta.