Bahrain, Israel zaongoza kuwa na wafungwa wengi wa kisiasa duniani
Mbunge wa zamani wa Bahrain amesema nchi hiyo ya Kiarabu ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wafungwa wengi wa kisiasa duniani.
Jalal Firouz ameyasema hayo leo Jumatatu katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kufafanua kuwa, utawala wa Aal-Khalifa unawazuilia wafungwa wa kisiasa zaidi ya elfu tano, na hivyo kuifanya Bahrain kijiografia na kutokana na idadi ndogo ya watu, kuwa nchi inayowazuilia wafungwa wengi wa kisiasa duniani, hususan wakosiaji wa serikali.
Amesema hali katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi hivi sasa ni ya kutisha na vyombo vya usalama vinashadidisha ukanamizaji wao kila uchao.
Tangu Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao, ikiwemo kutumia mbinu ya kamatakamata dhidi ya wapinzani na wakosaji wake.
Mbunge huyo wa zamani wa Bahrain ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unashika nafasi ya pili duniani, kwa kuwa na wafungwa wengi wa kisiasa.