Jul 10, 2018 13:47 UTC
  • Assad: Syria yaanzisha mkakati wa ujenzi mpya baada ya magaidi kutimuliwa

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kipaumbele chake ni ujenzi mpya wa nchi hiyo baada ya kutimuliwa magaidi walioanzisah vita nchini humo mwaka 2011 kwa uungaji mkono wa kigeni.

Rais Assad ameyasema hayo mjini Damascus wakati alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Walid al Muallem aliyeandamana na wanadiplomasia wa Syria katika nchi za kigeni.

Assad amesema sambamba na ujenzi mpya, Syria pia itaendelea kukabiliana na ugaidi nchini humo. 

Vita vya zaidi ya miaka saba Syria vimeharibu miundo msingi ya nchi hiyo hasa mitandao ya umeme na maji, shule, mahospitali na taasisi nyinginezo ambazo ni muhimu kwa ajili ya maisha ya kila siku.

Mwaka 2017, Benki ya Dunia ilikadiria kuwa Syria imepata hasara ya dola bilioni 226 kutokana na vita. Rais Assad amekadiria kuwa nchi hiyo kwa uchache inahitaji dola bilioni 200 huku akisisitiza kuwa hatakubali michango ya madola ya Magharibi.

Wanajeshi wa Syria wakiwa katika moja ya maeneo waliyokomboa kutoka makucha ya magaidi

Katika mahojiano na Televisheni ya NTV ya Russia mwezi Juni, Assad alisema nchi za Magharibi hazitahusishwa katika ujenzi mpya wa Syria hata zikitangaza kuwa tayari kutoa mchango. 

Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya magaidi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, Utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na waitifaki wao kuanzisha mashambulio kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais Bashar al-Assad. Hata hivyo kusimama kidete jeshi la Syria na waitifaki wake mbele ya njama dhidi ya taifa hilo  kumesambaratisha njama za maadui hao na kuvuruga mahesabu yao yote.

Tags