Msemaji wa shirika la UNRWA: Ghaza imekuwa jela kubwa
(last modified Sun, 15 Jul 2018 13:45:38 GMT )
Jul 15, 2018 13:45 UTC
  • Msemaji wa shirika la UNRWA: Ghaza imekuwa jela kubwa

Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) amesema kuwa eneo la Ukanda wa Ghaza limegeuka na kuwa jela kubwa isiyo na uthabiti na kwamba wakazi wa eneo hilo hawana cha kupoteza.

Akizungumza na gazeti la Kizayuni Yediot Aharanot, Adnan  Abu Hasna amesema kuwa raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Ghaza wana hali mbaya ya kiuchumi ambayo katika miezi ya karibuni imekuwa ikizingatiwa katika uga wa kimataifa. 

Mshauri huyo wa masuala ya habari wa shirika la Unrwa amesisitiza kuwa  uharibu uliosababishwa katika vita vya siku 50 huko Ghaza mwaka 2014 bado haujafanyiwa ukarabati huku asilimia 50 ya jamii ya watu milioni mbili wa Ukanda wa Ghaza wakiwa hawana ajira. Aidha amesema sekta binafsi katika eneo hilo imekufa kabisa. 

Maafa na uharibu baada ya vita vya siku 50 katika Ukanda wa Ghaza 

Kuhusu kupungua misaada ya kifedha ya kila mwaka ya Marekani kwa shirika hilo, Adnan Abu Hasna amesema kuwa Unrwa kila mwaka hupokea msaada wa fedha wa dola milioni 360, hata hivyo mwaka huu shirika hilo limepokea dola milioni sitini pekee; ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo ni kwa ajili ya kununulia bidhaa za chakula. Ameongeza kuwa shirika la Unrwa kila miezi mitatu huandaa chakula kwa Wapalestina milioni moja wa Ukanda wa Ghaza. Amesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa hivi sasa halina fedha zozote za kuendelea kutoa misaada ya chakula kwa raia wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza na kwamba hali ya mambo katika eneo hilo imeendelea kuwa mbaya.