Kamisheni ya UN: Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza
Tume huru ya Umoja wa Mataifa imeutuhumu utawala wa Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki kwa kuwashambulia raia wa Kipalestina wanaohifadhiwa katika shule na maeneo ya kidini huko Gaza.
Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu jana Jumanne iliushutumu utawala wa Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari kwa kuwalenga raia waliotafuta hifadhi kwenye maskuli na maabadi huko Gaza.
Tume hiyo, inayoongozwa na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, itawasilisha matokeo kamili ya uchunguzi wake kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva mnamo Juni 17, 2025.
"Israel imeharibu mfumo wa elimu wa Gaza na kuharibu zaidi ya nusu ya maeneo yake ya kidini na kitamaduni," Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema katika ripoti yake. Jopo hilo la watu watatu limevishutumu vikosi vya Israel kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia na kufanya mauaji kwa makusudi katika vituo vya elimu.
"Katika kuwalenga raia wanaojihifadhi katika shule na maeneo ya kidini, vikosi vya usalama vya Israel vimefanya uhalifu dhidi ya binadamu (kwa lengo la) kuwaangamiza," imehitimisha ripoti hiyo. "Kuna ushahidi unaoongezeka kwamba Israel inafanya kampeni ya makusudi na ya kimfumo ya kufuta maisha ya Wapalestina huko Gaza," amesema Pillay katika taarifa hiyo.
Licha ya raia wa Palestina kuendelea kuuawa kinyama kila leo na hata kutolewa indhari chungu nzima za mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu njaa huko Gaza, lakini serikali za Magharibi zimekataa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya jinai za Israel.