Bahrain yawafutia uraia mamia ya wanaharakati wa asasi za kiraia
Utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain umewafutia uraia wanaharakati 738 wa asasi za kiraia wa nchi hiyo.
Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limeinukuu taasisi moja ya kisheria ya Bahrain na kueleza kuwa tangu mwaka 2012 hadi sasa utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia wanaharakati 738 wa nchi hiyo. Mwaka huu pia utawala huo umewafutia uraia Wabahraini 232.
Eric Goldstein Naibu Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kanda ya katika Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuwafutia uraia idadi hiyo ya wananchi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na Manama inapasa kuwarejeshea wananchi hao uraia wao.
Wananchi wa Bahrain walianzisha harakati za mageuzi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa Februari 14 mwaka 2011 wakitaka kung'oka madarakani utawala huo na kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa. Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa siasa hizo za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa na kutoa wito wa kufanyika marekebisho katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo.