Majibu makali ya Wapalestina kwa mashambulizi ya Wazayuni Ukanda wa Ghaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na brigedi za Quds, tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina mapema jana asubuhi (Alkhamisi) zilitoa matamko tofauti ya kusisitizia haki yao ya kujilinda mbele ya uvamizi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Makundi ya Wapalestina ya Hamas na Jihadul Islami yamesema bayana kuwa muqawama wa taifa la Palestina utaendelea kujibu mashambulizi ya adui Mzayuni kwa kutumia msingi wa "mshambulie anayekushambulia." Taarifa za makundi hayo ya Palestina zimetolewa baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mashambulizi makubwa katika Ukanda wa Ghaza. Makundi ya wanamapambano wa Palestina yamelazimika kujibu uvamizi huo wa Wazayuni kwa kushambulia kwa makombora 100 vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, sababu kuu iliyoupa kiburi utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuushambulia Ukanda wa Ghaza, ni siasa za kibeberu za rais wa Marekani, Donald Trump. Siasa za Trump za kuwaunga mkono kila upande Wazayuni ndizo zinazowafanya wavamizi hao wa Kibla cha Kwanza cha Waislamu kufanya jinai wanazotaka huko Palestina. Kwa mfano hivi sasa rais wa Marekani amekuja na mpango wa "Mapatano ya Karne" kwa lengo la kuuunga mkono kila upande utawala wa Kizayuni wa Israel na kuliangamiza kikamilifu taifa la Palestina. Lengo la Trump ni kusahaulisha kikamilifu malengo matukufu ya Palestina ikiwa ni pamoja na haki ya wakimbizi wa Kipalestina ya kurejea katika ardhi za mababu zao zilizotekwa na Wazayuni na kupachikwa jina bandia la Israel. Hata hivyo tangu tarehe 30 Machi mwaka huu, wananchi wa Palestina wamekuwa wakiendelea na maandamano yao ya kupigania haki ya kurejea katika ardhi zao suala ambalo limefelisha njama za maadui za kujaribu kulisahaulisha suala la Palestina. Kuendelea maandamano ya Wapalestina hao kwa miezi mingi sasa kumewatia kiwewe maadui hasa Marekani na baada ya utawala wa Kizayuni kuona kuwa umeshindwa kuzima maandamano hayo ya Wapalestina, umeamua kuanzisha chokochoko nyingine za kufanya mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza ili kuficha kushindwa kwake kukabiliana na maandamano ya Wapalestina.
Hata hivyo matukio ya Palestina ni uthibitisho wa wazi kuwa kambi ya muqawama hivi sasa imo katika mazingira mazuri ya kuweza kutumia stratijia ya kumshambulia anayekushambulia na kutotoa mwanya kwa adui wa kuthubutu kushambulia kirahisi bila ya kupata majibu ya mashambulizi yake. Hatua ya makundi ya muqawama ya Palestina ya kujibu mashambulizi kwa kuyapiga maeneo ya Wazayuni kumeonesha wazi kuwa Wapalestina hawatishwi na mashambulizi ya Wazayuni bali ni Wazayuni wapenda dunia ndio wanaopaswa kutishwa na majibu ya wanamapambano wa Palestina.
Ukweli huo unabainishwa wazi na mkuu wa zamani wa ujasusi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni ambaye amesema: "Majibu ya moto ni moto" ndio mlingano mpya wa kijeshi ambao makundi ya Palestina huko Ghaza yameitwisha Israel na ndilo tunalolishuhudia hivi sasa ambapo Israel inashambulia na Wapalestina wanajibu mtawalia.
Kutokea awamu mpya ya Intifadha ya wananchi wa Palestina ambayo imezitikisa nguzo zote za utawala wa Kizayuni wa Israel ni uthibitisho wa wazi kuwa wavamizi hao wa Quds hawawezi kujilinda na vipigo vya muqawama wa Palestina popote pale wanapojificha. Matukio ya hivi sasa ya Palestina yanaonesha kuwa mapambano ya wananchi wa taifa hilo yameingia kwenye hatua madhubuti zaidi na hizo ni kengele za hatari kwa utawala wa Kizayuni ambao ulikuwa katika wakati mgumu pia kwenye Intifadha za huko nyuma. Nukta muhimu hapa ni kuwa Israel imeshindwa kuzima maandamano ya Wapalestina na majibu makali yaliyotolewa na makundi ya mapambano ya Palestina ya Hamas na Jihadul Islami ni ushahidi mwingine wa azma thabiti ya Wapalestina ya kuendelea kupigania haki zao kwa namna yoyote ile.