Hashdu Sha'abi: Marekani ndio inayochochea ghasia Basra, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47992-hashdu_sha'abi_marekani_ndio_inayochochea_ghasia_basra_iraq
Kamanda wa ngazi za juu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi nchini Iraq cha Hashdu Sha'abi amesema harkati hiyo ya wananchi tayari imewakabidhi maafisa wa serikali ya Baghdad ushahidi unaoonesha kuwa ubalozi mdogo wa Marekani mjini Basra ndio uliohusika katika kuratibu na kuchochea machafuko yanayoendelea kushuhudiwa hivi sasa katika mkoa wa Basra, kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2018 07:12 UTC
  • Hashdu Sha'abi: Marekani ndio inayochochea ghasia Basra, Iraq

Kamanda wa ngazi za juu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi nchini Iraq cha Hashdu Sha'abi amesema harkati hiyo ya wananchi tayari imewakabidhi maafisa wa serikali ya Baghdad ushahidi unaoonesha kuwa ubalozi mdogo wa Marekani mjini Basra ndio uliohusika katika kuratibu na kuchochea machafuko yanayoendelea kushuhudiwa hivi sasa katika mkoa wa Basra, kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Sanjari na kulaani uwepo wa askari 8,000 wa Marekani nchini humo na uingiliaji wa masuala ya ndani wa Washington kwa nchi hiyo ya Kiarabu, Naibu Kamanda wa Hashdu Sha'abi, Abu Mahdi al-Muhandis amesema Marekani ilikuwa imetoa vitisho hapo awali kuwa mji wa Basra 'ungeteketezwa kwa moto' iwapo Waziri Mkuu wa sasa hatashinda muhula wa pili.

Kamanda huyo wa harakati ya Hashdu Sha'abi  kadhalika amemkosoa Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq kwa kukataa kuviunga mkono vikosi hivyo vya kujitolea vya wananchi sambamba na kuilimbikizia tuhuma mbalimbali.

Ubalozi mdogo wa Iran mkoani Basra ulioteketezwa moto na kundi la waandamanaji

Hapo juzi, Sheikh Qais Khazali, Katibu Mkuu wa kundi la Asa'ib Ahl al-Haq ambalo ni sehemu ya Hashdu Sha'abi nchini Iraq, alisema kuwa watu wanaofanya ghasia katika mkoa wa Basra, wanatekeleza malengo maalumu ya Washington kupitia maandamano, huku akihoji ni kwa nini waandamanaji hao hawakushambulia balozi ndogo za Marekani mjini humo.

Ijumaa usiku, kundi la waandamanaji liliiteketeza kwa moto jengo lenye ubalozi mdogo wa Iran mkoani Basra. Kabla ya hapo, waandamanaji hao waliyashambulia pia majengo ya serikali, mashirika ya kiraia na makundi ya kisiasa.