Iran: Madai ya US dhidi yetu kuhusu Basra hayana msingi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48097-iran_madai_ya_us_dhidi_yetu_kuhusu_basra_hayana_msingi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madai ya Marekani kwamba Tehran imehusika katika machafuko ya mji wa Basra nchini Iraq ni ya kipuuzi, ya kichochezi na yasiyokuwa na msingi.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Sep 13, 2018 02:39 UTC
  • Iran: Madai ya US dhidi yetu kuhusu Basra hayana msingi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madai ya Marekani kwamba Tehran imehusika katika machafuko ya mji wa Basra nchini Iraq ni ya kipuuzi, ya kichochezi na yasiyokuwa na msingi.

Bahran Qassemi aliyasema hayo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari mjini Tehran na kuongeza kuwa, lengo la madai hayo ya Marekani ni kujaribu kupotosha fikra za walimwengu ambao wanafahamu fika kuwa Washington ndiyo inayobeba dhima ya uharibifu wote nchini Iraq.

Amesema sera za Marekani dhidi ya Iraq na uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ndilo chimbuko la ukosefu wa usalama na uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Siku ya Jumanne, Katibu wa Vyombo vya Habari wa Ikulu ya Marekani White House alidai kuwa, vikosi vinavyoungwa mkono na Iran nchini Iraq vimefanya mashambulizi ya kutisha dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Basra na dhidi ya ubalozi wa Washington mjini Baghadad.

Ubalozi mdogo wa Iran ulioteketezwa moto mjini Basra

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Marekani inapaswa kuwajibishwa kutokana na hatua yake ya kuunga mkono makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kuchupa mipaka sio tu Iraq bali katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Ijumaa usiku, kundi la waandamanaji liliteketeza kwa moto jengo la ubalozi mdogo wa Iran mkoani Basra. Kabla ya hapo, waandamanaji hao waliyashambulia pia majengo ya serikali, mashirika ya kiraia na makundi ya kisiasa.