Hamas yaionya Israel isiendelee kukivunjia heshima Kibla cha Kwanza cha Waislamu
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel juu ya hatari ya kuendelea kuuvinjia heshima Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu na kusisitiza kuwa utawala huo dhalimu ndio utakaobeba dhima ya lolote litakalotokea.
Katika tamko lake la jana Alkhamisi, harakati ya HAMAS ilisema kuwa, kitendo cha walowezi wa Kizayuni cha kuzidi kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa katika siku za hivi karibuni kinaonesha kuwa Israel ina nia ya kuudhibiti msikiti huo na kutekeleza ngano za Kizayuni kuhusu eneo hilo takatifu.
Vile vile harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu imesema kuwa, hatua ya walowezi wa Kizayuni ya kuzidi kukivunjia heshima Kibla cha Kwanza cha Waislamu ni katika kutekeleza mpango haramu wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na kulishinikiza kila upande taifa la Palestina, hivyo imewataka Waislamu na wapenda haki wote hususan Wapalestina kujitokeza kwa wingi kukabiliana na njama hizo za Marekani na Israel.
Aidha imezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kutekeleza majukumu yao ya kukilinda Kibla cha Kwanza cha Waislamu na kuonesha hasira zao dhidi ya jinai za kila uchao za utawala wa Kizayuni. Taarifa ya harakati hiyo ya Kiislamu imesema: Nchi za Kiarabu na Kiislamu zinapaswa kuunganisha nguvu zao kukabiliana na adui yao wa pamoja nao ni utawala wa Kizayuni wa Israel ulioziteka na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Waislamu.
Katika siku za hivi karibuni, walowezi wa Kizayuni wamezidisha uvamizi wao ndani ya Msikiti wa al Aqsa na jambo hilo limewakasirisha Wapalestina wanaoishi Baytul Muqaddas, makundi ya Kipalestina pamoja na duru mbalimbali za Kiislamu na Kiarabu.