HAMAS: Matamshi ya Mahmoud Abbas yanabainisha mtazamo wake binafsi
Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuhusu matamshi aliyotoa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuwa tayari kufanya mazungumzo na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, kwamba matamshi hayo yanaakisi mtazamo wake binafsi, wala hayawakilishi maoni ya wananchi wa Palestina.
Katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mjini Paris, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema yuko tayari kuanza mazungumzo mapya ya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa siri au hadharani kupitia mpatanishi wa kimataifa.
Msemaji wa HAMAS, Sami Abu Zuhri ameandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba: Matamshi ya Mahmoud Abbas yanadhihirisha jinsi upinzani wake kwa mpango wa "Muamala wa Karne" usivyo na itibari wala thamani yoyote na ni sawa na kutoa pigo kwa wananchi wa Palestina wanaoandamwa kila uchao na hujuma na mashambulio ya Israel.
Mahmoud Abbas ametoa kauli hiyo katika hali ambayo serikali ya Marekani imechukua hatua kadhaa kwa lengo la kuuhami na kuunga mkono kwa kila hali utawala wa Kizayuni wa Israel na mpango uitwao "Muamala wa Karne". Miongoni mwa hatua hizo ni kuuhamishia Quds tukufu ubalozi wake wa Tel Aviv na hivi karibuni kabisa kuamua kukata misaada yake ya kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.../