Israel yakerwa baada ya Madrid kumuenzi mwanaharakati wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48496-israel_yakerwa_baada_ya_madrid_kumuenzi_mwanaharakati_wa_palestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeghadhabishwa mno na hatua ya klabu mashuhuri ya soka ya Uhispania ya Real Madrid kumuenzi kwa kumtunuku jezi nambari 9 Ahed Tamimi, binti mwanamapambano wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 01, 2018 02:39 UTC
  • Israel yakerwa baada ya Madrid kumuenzi mwanaharakati wa Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeghadhabishwa mno na hatua ya klabu mashuhuri ya soka ya Uhispania ya Real Madrid kumuenzi kwa kumtunuku jezi nambari 9 Ahed Tamimi, binti mwanamapambano wa Kipalestina.

Emanuel Nachshon, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Ni aibu ilioje kwa Real Madrid kumpokea gaidi ambaye anachochea chuki na ghasia. Kuna uhusiano gani kati ya hilo na mpira wa miguu?

Ofisa mwingine wa utawala haramu wa Israel aliyeonesha kuingiwa na kiwewe kwa kitendo hicho cha Madrid kumuenzi mwanaharakati huyo wa Palestina ni Daniel Kutner, balozi wa Israel nchini Uhispania ambaye ameandika: Ahed Tamimi sio mtetezi wa amani, ni mtu anayeunga mkono ghasia na ugaidi. Taasisi zilizompokea na kumtunuku zinaunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja uvamizi na machafuko na wala sio mazungumzo na maelewano tunayopigania. 

Ahed Tamimi ambaye kwa sasa amekuwa nembo ya muqawama katika ardhi za Palestina, anazitembelea nchi za Ulaya baada ya kuachiwa huru na jeshi la utawala haramu wa Israel.

Tamimi akiongea na waandishi wa habari

Itakumbukwa kuwa askari wa utawala katili wa Kizayuni walimkamata Ahed, tarehe 19 Septemba mwaka jana kwa tuhuma za kumshambulia askari wa utawala huo vamizi, huku akiachiliwa huru tarehe 29 Julai mwaka huu,  baada ya kubakia jela kwa miezi minane.

Awali msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 na ambaye amegeuka kuwa nembo ya muqawama, alielezea uwezekano wa kusafiri nchini Iran kwa kusema, licha ya vizuizi vingi vya Israel vinavyomzuia kuelekea Iran likiwemo tishio la kumrejesha jela, lakini Tel Aviv haiwezi kuzuia malengo yake ya kimuqawama.