Israel yaazimia kuwabana zaidi wafungwa wa Kipalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48741-israel_yaazimia_kuwabana_zaidi_wafungwa_wa_kipalestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel unatazamiwa kushadidisha mateso na kuwawekea mbinyo zaidi wafungwa wa Kipalestina unaowazuilia katika jela zake za kuogofya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 12, 2018 07:42 UTC
  • Israel yaazimia kuwabana zaidi wafungwa wa Kipalestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatazamiwa kushadidisha mateso na kuwawekea mbinyo zaidi wafungwa wa Kipalestina unaowazuilia katika jela zake za kuogofya.

Kamati maalumu iliyoundwa na Gilad Erdan, Waziri wa Usalama wa Umma wa utawala huo haramu inatazamiwa kukabidhi ripoti yake yenye mapendekezo ya kuwabana zaidi wafungwa wa Kipalestina, kukiwemo kupunguza siku za wafungwa hao kutembelewa na familia zao, kutoruhusiwa kupika wala kuletewa bidhaa kama nyama, matunda, samaki na mboga za majani, mbali na kuangalia upya hukumu ya eti watuhumiwa wa ugaidi, ambao hukumu ya chini sasa itakuwa kifungo cha miaka 60 jela kutoka 40. 

Akizindua kamati hiyo mwezi Juni mwaka huu, waziri huyo wa utawala pandikizi  wa Israel alisema, lengo haswa la kubuniwa kamati hiyo ni kuzishinikiza harakati za mapambano za Palestina kama vile Hamas, ziukabidhi utawala huo mabaki ya askari wa Israel wanaozuiliwa katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Kamati ya Wafungwa iliyo chini ya usimamizi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO na Jumuiya ya Asir ambayo inashughulikia masuala ya wafungwa wa Palestina, tokea mwaka 1967 hadi sasa, wafungwa wapatao 214 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika jela za kuogofya za utawala haramu wa Israel.

Askari wa Israel wakimteka nyara kijana wa Kipalestina

Kwa mujibu wa takwimu mpya rasmi, hivi sasa kuna zaidi ya Wapalestina 6500 wanaoteseka katika jela hizo za kutisha, wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Siasa za utawala huo za kuteka nyara na kuwafunga Wapalestina katika jela zake za kuogofya zimepelekea Wapalestina zaidi ya milioni moja kuzuiwa katika jela hizo katika kipindi cha miongo mitano iliyopita, na hivyo kufanya idadi kubwa ya Wapalestina kupitishia maisha yao au sehemu kubwa ya maisha yao katika jela hizo.