Kuangamizwa ugaidi ndicho kipaumbele kikuu cha serikali mpya ya Iraq
Jumamosi iliyopita Waziri Mkuu mpya wa Iraq, Adil Abdul-Mahdi alikutana na viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa kijeshi na kiusalama nchini humo ambapo alisisitizia ulazima wa kuendelezwa mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi hadi kukatwa kibisa mizizi yake.
Sambamba na kubainisha kwamba wadhifa wa jeshi na vikosi vya usalama ni kulinda wananchi, Abdul-Mahdi amesema kwamba kujitolea kwa vikosi vya Iraq ndiko kumeifanya nchi hiyo kupata ushindi dhidi ya ugaidi. Itakumbukwa kuwa kundi la kigaidi la Daesh kwa uungaji mkono mkubwa wa kigeni na ndani, liliivamia Iraq mwaka 2014 ambapo katika kuonyesha uwezo wake lilidhibiti maeneo makubwa ya kaskazini na magharibi mwa nchi sambamba na kutekeleza jinai zisizo na idadi katika maeneo hayo. Mwanzoni mwa wanachama wa kundi hilo kuingia Iraq, walidhani kwamba wangeweza kuidhibiti kikamilifu nchi hiyo, hata hivyo uelewa wa maraajii, wananchi na viongozi wa serikali ya Iraq, ulipelekea kuundwa safu umoja dhidi ya wanachama wa kundi hilo hatari la ukufurishaji. Umoja wa kupigiwa mfano wa Wairaki ulikuwa sababu ya kuzuiwa upenyaji wa kundi hilo hatari nchini kwao.

Katika anga hiyo, vikosi vya kujitolea vya wananchi (Hashdu sh-Sha'abi) viliweza kuundwa kupitia fatwa ya Ayatullah Sayyid Sistatani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia nchini humo, kutoka makundi tofauti ya Iraq. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia kudhibitiwa mji wa Mosul na wanachama wa Daesh (ISIS) hapo tarehe 10 Juni 2014. Ushirikiano wa wananchi, jeshi na serikali, ilikuwa sababu chanya iliyopelekea kudhoofishwa kundi hilo. Uono wa mbali wa viongozi wa ngazi za juu wa Iraq kuhusu nafasi athirifu ya harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi, jeshi na serikali, uliwafanya watangaze wazi mwaka wa 2017 na 2018 kuwa wakati wa kusambaratishwa kundi la Daesh nchini Iraq . Inafaa kuashiria kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, magaidi wakufurishaji wamepata pigo kubwa nchini Iraq, hata hivyo ushindi wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya hatari hiyo hauna maana kwamba magaidi hao wamemalizwa kikamilifu. Kwa ibara nyingine ni kwamba kwa mtazamo wa kijeshi, genge la Daesh limefikia tamati, hata hivyo kunaibuka swali hili kwamba je, baada ya hapo Wairaki watakuwa salama kutokana na shari ya ugaidi? Au kwamba kundi hilo la ukufurishaji na Kiwahabi litaendeleza hujuma zake kwa njia nyingine tofauti na hivyo kuhatarisha maisha ya raia na usalama wa taifa kwa ujumla?

Hadi sasa harakati ndogondogo za makundi ya kigaidi zinazoendelea kushuhudiwa katika maeneo tofauti ya Iraq na ambazo zimekuwa zikitekelezwa kupitia mashambulizi ya kuvizia ya kigaidi, zinabainisha kwamba magaidi hao bado ni hatari kwa usalama wa nchi hiyo ya Kiarabu. Na hasa tukizingatia kuwa wanakusudia kujiimarisha upya kupitia misaada ya waungaji mkono wao wa kigeni, yaani madola ya Magharibi na watawala vibaraka wa Kiarabu na kupitia ombwe la usalama kwa ajili ya kuzusha wimbi jipya la ugaidi nchini humo. Ukweli ni kwamba kundi la Daesh baada ya kushindwa katika medani ya vita, linatumia mbinu mpya kuvuruga usalama wa Iraq kupitia mauaji ya kuvizia na utegaji mabomu. Matukio ya Iraq yanaonyesha kwamba ushindi wa jeshi dhidi ya wanachama wenye misimamo mikali ya kigaidi bado haujafika mwisho na ni lazima kukatwa kikamilifu mizizi ya wimbi hilo. Katika mazingira hayo aina mpya ya mapambano baada ya kumalizika vita vya mtutu wa bunduki, ni lazima kuendelee vita vya intelejensia, si kupitia askari pekee, bali kupitia pia intelejensia inayojumuisha utamaduni kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kusambaratisha fikra za usalafi wa Kiwahabi. Katika mazingira hayo sambamba na matumaini ya kukatwa mizizi ya ugaidi, kuingia katika hatua mpya ya baada ya Daesh, kunahitajia ukarabati na ustawi wa kiuchumi na kisiasa, mambo ambayo yameashiriwa pia na Waziri Mkuu mpya wa Iraq, Adil Abdul-Mahdi.