Viongozi wa Kikristo mjini Quds wakosoa ubaguzi wa Netanyahu
Wakuu wa Kanisa Katoliki katika mji wa Quds tukufu unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel wamemuandikia barua Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu wakikosoa misimamo yake ya kibaguzi.
Viongozi hao wa Kikristo mjini Quds wamesema sheria ya kibaguzi iliyopasishwa hivi karibuni na utawala huo wa Kizayuni inakiuka haki za binadamu na misingi ya utu.
Katika barua hiyo, Wakuu wa Kanisa Katoliki katika mji wa Quds tukufu wamemtaka Benjamin Netanyahu kuangalia upya sheria hiyo inayowafadhilisha Mayahudi na kuwadhalilisha Waislamu na Wakristo, sambamba na kuwanyima fursa za kuyazuru maeneo matukufu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka huu, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliupasisha muswada wa sheria inayotaka kutambuliwa Israel kama 'dola la Mayahudi pekee' licha ya upinzani mkali na malalamiko kutoka kila pembe ya dunia.
Mbali na sheria hiyo kuzifadhilisha 'thamani za Kizayuni' badala ya 'thamani za kidemokrasia' katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, lakini pia inautambua Quds kama mji mkuu wa Israel, sanjari na kukitambua Kiebrania kama lugha rasmi na kukitweza Kiarabu.
Mwezi uliopita, Katika makala yake iliyochapishwa kwenye gazeti la Guardian la Uingereza, Nkosi Zwelivelile Mandela, mjukuu wa shujaa wa uhuru wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela amefananisha mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya waandamanaji wa Palestina huko katika Ukanda wa Gaza na mauaji yaliyofanywa na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini katika eneo la Sharpeville mwaka 1960 na kusisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni mbaya zaidi kuliko ule wa apartheid.