Wapinzani wanne wa utawala wa Bahrain kunyongwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49472-wapinzani_wanne_wa_utawala_wa_bahrain_kunyongwa
Mahakama nchini Bahrain imepitisha hukumu ya kunyongwa raia wanne wa nchi hiyo ambao ni wapinzani wa utawala wa kifalme unaoongozwa na ukoo wa Aal Khalifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2018 23:21 UTC
  • Wapinzani wanne wa utawala wa Bahrain kunyongwa

Mahakama nchini Bahrain imepitisha hukumu ya kunyongwa raia wanne wa nchi hiyo ambao ni wapinzani wa utawala wa kifalme unaoongozwa na ukoo wa Aal Khalifa.

Taarifa zinasema wapinzani hao wanne wanatuhumiwa kuhusika na utegaji bomu mwaka jana na kwa msingi huo mahakama imewahukumu kifo huku utawala wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi ukiendelea na kampeni ya kuwakandamiza wapinzani.

Hayo yanajiri siku chache baada ya Mahakama ya Bahrain kumhukumu kifungo cha maisha jela Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa harakati ya kitaifa na Kiislamu ya nchi hiyo ya Al-Wifaq.

Baada ya kutolewa hukumu hiyo, harakati ya Al-Wifaq imetoa taarifa na kutangaza kuwa: Wananchi wa nchi hiyo wana uelewa zaidi wakati huu kuliko wakati wowote ule kuhusu ulazima wa kubadilishwa utawala nchini Bahrain.

Sheikh Ali Salman

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yamemtaja Sheikh Ali Salman pamoja na viongozi wengine wa upinzani wanaotumikia vifungo jela nchini Bahrain kuwa ni watu waliofungwa jela kwa sababu ya imani zao.

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain inashuhudia vuguvugu la mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka utawala huo wa ukoo wa kifalme uondoke madarakani na wafungwa wote wa kisiasa waachiwe huru.