Makubaliano ya usitishaji vita yamfanya Waziri wa Vita wa Israel ajiuzulu
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Avigdor Liberman ametangaza kujiuzulu wadhifa wake eti kulalamikia hatua ya harakati za mapambano za Palestina ikiwemo Hamas kufikia makubaliano ya kusitisha vita na utawala huo dhalimu katika Ukanda wa Gaza kupitia upatanishi wa Misri.
Lieberman amedai kuwa, Israel kusaini makubaliano hayo ya usitishaji vita ni sawa na kusalimu amri mbele ya ugaidi. Kadhalika amesema amelazimika kujiuzulu kulalamikia hatua ya utawala huo haramu kukubali Qatar itume dola milioni 15 za Marekani katika Ukanda wa Gaza, kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wa serikali na watumishi wa umma.
Hata hivyo viongozi wa Palestina akiwemo Sami Abu Zuhri, msemaji wa Hamas amesema hatua ya Lieberman kujiuzulu ni sawa na Israel kukubali kushindwa na wanamuqawama wa Palestina, na pia ni ushindi mkubwa wa kisiasa kwa Wapalestina wa Gaza, ambao wamesimama kidete mbele ya uvamizi na uporaji wa ardhi wa utawala ghasibu wa Israel.
Aidha amesisitiza kuwa, harakati za mapambano za Palestina zitaheshimu makubaliano hayo ikiwa tu utawala huo khabithi hautayakiuka.
Askari wa kikosi maalumu cha utawala wa Kizayuni, Jumapili iliyopita waliijipenyeza hadi mashariki ya mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza na kufanya mauaji ya kigaidi kwa kuwaua shahidi makamanda wawili wa brigedi ya Izzuddin Al-Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas na Wapalestina wasiopungua wanane.
Harakati za mapambano za Palestina alfajiri ya Jumatatu zilijibu mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuvishambulia kwa makombora vitongoji zaidi ya 50 vya walowezi wa Kizayuni na vituo kadhaa vya askari wa Israel.