Wanazuoni Afghanistan waharamisha kilimo cha mpopi na uzalishaji wa dawa za kulevya
Wanazuoni wa Kiislamu wa wilaya 22 za mkoa wa Nangarhar nchini Afghanistan wametangaza kuwa, kilimo cha zao la mpopi, uzalishaji wa dawa za kulevya na utumiaji wake ni haramu na kinyume na sheria za dini ya Kiislamu.
Tangazo hilo limetolewa katika kikao cha wanazuoni hao kilichofanyika katika mji wa Jalalabad ambao ni makao makuu ya mkoa wa Nangarhar huko mashariki mwa Afghanistan. Wanazuoni hao wameahidi kwamba, watatumia misikiti kuwaelimisha wananchi kwamba, kilimo cha zao la mpopi linalotumiwa kuzalisha dawa za kulevya na utumiaji wa dawa hizo ni haramu.
Maafisa wa Wizara ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Afghanistan daima wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa mchango wa wanazuoni wa kidini katika kupambana na kilimo cha mpopi na uzalishaji wa dawa za kulevya na kusema kuwa, kuna umuhimu wa kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya dawa hizo.
Baada ya Marekani kuivamia Afghanistan mwaka 2001 kilimo cha mpopi na dawa za kulevya kiliongezeka kwa kiwango kikubwa nchini humo na takwimu za taasisi za Marekani zinasema kuwa, kwa sasa karibu hektari laki 8 na 20 elfu za ardhi ya nchi hiyo zinatumiwa kwa ajili ya kilimo cha mpopi. Hii ni licha ya kuwa, serikali ya Afghanistan imetumia njia na mbinu zote zinazowezekana kuzuia kilimo cha zao hilo linalotumiwa kuzalisha dawa za kulevya aina ya heroin. Hata hivyo ukosefu wa ushirikiano wa askari vamizi wa Marekani na waitifaki wao katika uwanja huo umekwamisha mikakati yote ya kupambana na kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan. Suala hilo linaifanya Afghanistan kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa dawa za kulevya duniani.
Tunapaswa kuashiria nukta kadhaa kuhusu suala la kuongezeka uzalishaji wa zao la mpopi nchini Afghanistan. Kwanza ni kwamba, katika kipindi chote cha miongo miwili ya uvamizi wa Marekani na washirika wake huko Afghanistan hakujaainishwa zao mbadala la mpopi kwa ajili ya wakulima wa nchi hiyo. Japokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwanzoni mwa kuundwa serikali ya Afghanistan ilipendekeza zao mbadala kama njia ya kupambana na dawa za kulevya nchini humo lakini Marekani na duru za kimataifa hazikuunga mkono pendekezo hilo.
Ahmad Nasiir Tareki ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: Kutokuwepo irada ya kisiasa ya kupambana na kilimo cha mpopi, ukosefu wa misaada kwa wakulima, ushirikiano wa wahalifu wa ndani na wafanya magendo wa kigeni na ukosefu wa amani na usalama ndizo sababu kuu zinazochangia ongezeko la uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan.
Sababu ya pili ya ongezeko la uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan ni kwamba, magendo ya dawa hizo inatambuliwa kuwa chanzo kikuu cha fedha cha makundi ya kigaidi na yale yenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini humo. Makundi hayo yanadhibiti maeneo mbalimbali ya Afghanistan na yanasimamia kilimo cha mpopi na uzalishaji wa dawa za kulevya na hata kuwatoza ushuru na kodi wakulima na wazalishaji wa dawa hizo.
Sababu ya tatu ya ongezeko la dawa za kulevya nchini Afghanistan ni utumiaji wa zana za kisasa katika kuzalisha dawa hizo, suala ambalo linaakisi ushirikiano mkubwa ulipo baina ya wazalisha na magenge ya kimataifa. Ripoti mbalimbali pia zinaonesha kuwa, viwanja vya ndege vya Afghanistan vinavyodhibitiwa na askari vamizi hususan Wamarekani na Waingereza vinachangia sana katika megendo na usafirishaji wa dawa hizo kuelekea kwenye masoko ya kimataifa.
Alaa kulli hal, kwa kutilia maanani satuwa na ushawishi wa wanazuoni na maulamaa wa kidini baina ya wananchi, inatazamiwa kuwa, hatua ya wanazuoni hao ya kusisitiza tena uharamu wa dawa za kulevya itasaidia kupunguza uzalishaji wa dawa hizo na hatimaye kukomeshwa kabisa balaa hilo linalosababisha maafa makubwa ya binadamu.