Mshauri wa zamani: Saudia iliidhinisha mauaji ya Yassir Arafat
Aliyekuwa mshauri mwandamizi wa Yasser Arafat, Rais wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amefichua kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) hakufa kifo cha kawaida baada kuugua, bali aliuawa, na kwamba Saudi Arabia ndiyo iliyoidhinisha mauaji yake.
Bassam Abu Sharif ameyafichua hayo katika mahojiano ya kipekee aliyofanya na shirika la habari la Shehab na kufafanua kuwa, Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush aliwasiliana na maafisa wa ngazi za juu wa Saudi Arabia baada ya kufanya kikao na aliyekuwa Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Ariel Sharon, ambapo kadhia ya kutaka kuuawa kwa sumu Arafat ilijadiliwa na kisha Saudia ikaiidhinisha.
Abu Sharif amebanisha kuwa, serikali ya Riyadh ilitoa baraka kwa mauaji ya Yasser Arafat kwa kuwa ilimtazama kama kizingiti kwenye kile kilichotajwa kama Mpango wa Amani ya Nchi za Kiarabu, uliotaka mgogoro wa Palestina na Israel utatuliwe kwa kutambuliwa pande mbili hizo.
Mshauri huyo wa ngazi za juu wa zamani wa Arafat ameongeza kuwa, "Sharon alikutana na Bush katika Ikulu ya Marekani ya White House, na kumwambia kuwa hawezi tena kuendelea kumvumilia Arafat kwa sababu alikuwa anaongoza eti kikundi cha kigaidi cha Hamas, na kwamba operesheni zote za Hamas zilifanyika kwa baraka zake."
Yasser Arafat, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambaye pia alikuwa kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliaga dunia Novemba 11, mwaka 2004 katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa, kwenye mazingira ya kutatanisha, akiwa na umri wa miaka 74.
Mwaka 2012, Suha, mjane wa Arafat alifungua faili la mauaji ya mumewe katika mahakama moja nchini Ufaransa, akisisitiza kuwa rais huyo wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alipewa sumu kabla ya kufariki dunia katika hospitali ya kijeshi mjini Paris, mwaka 2004, ingawaje madaktari wa Ufaransa walidai kuwa aliaga dunia kutoka na kiharusi.