PLO yawataka Wapalestina kupambana na wanajeshi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50153-plo_yawataka_wapalestina_kupambana_na_wanajeshi_wa_israel
Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kimewataka wananchi wa Palestina kutokubali kudhalilishwa na wasimame imara kupambana na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 14, 2018 00:53 UTC
  • PLO yawataka Wapalestina kupambana na wanajeshi wa Israel

Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kimewataka wananchi wa Palestina kutokubali kudhalilishwa na wasimame imara kupambana na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, chama cha PLO na harakati ya Fat'h zimesema kuwa, kutokana na kushadidi mashambulizi ya wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, wakati umefika kwa wananchi wa Palestina kutoa majibu makali dhidi ya uvamizi huo wa Wazayuni.

Jana Alkhamisi kamati ya utendaji ya PLO iliitisha kikao cha kuzungumzia jinai za Israel hasa baada ya kuuliwa shahidi wananchi wasio na hatia wa Paelstina na mbali na kulaani vikali uvamizi wa mara kwa mara wa wanajeshi wa Israel katika miji na vijiji vya Wapalestina na kutiwa mbaroni raia pamoja na kutoa adhabu za umati dhidi ya wananchi wa Palestina hasa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, imewataka wananchi wa Palestina waendelee na harakati zao za kila upande kama njia ya kukabiliana na mashambulizi na jinai hizo za wanajeshi wa Israel.

Unyama wa wanajeshi katili wa Israel dhidi ya Wapalestina

 

Vile vile kamati hiyo imezitaka nchi za Kiarabu kukomesha siasa zao za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa upande wake, harakati ya Fat'h jana ilitoa tamko na kulionya jeshi la Israel na walowezi wa Kizayuni kuhusu mashambulizi na jinai zao dhidi ya wananchi wa Palestina.

Siku chache zilizopita pia, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS iliionya Israel na kusema kuwa ndiyo itakayobeba jukumu na lawama za baya lolote litakalomtokea Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina baada ya Wazayuni kutishia kumuua kutokana na msimamo wake wa kukataa kuorodheshwa HAMAS katika makundi ya kigaidi.