Palestina yaomba uanachama wa kudumu katika Umoja wa Mataifa
Riyad al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, Rais Mahmoud Abbas wa mamlaka hiyo mwezi ujao wa Januari ataelekea mjini New York Marekani kuwasilisha rasmi ombi la serikali ya Palestina kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuwa mwanachama wa kudumu wa umoja huo.
Shirika la habari la Ma'an la Palestina limeripoti habari hiyo na kumnukuu al Maliki akisema katika mahojiano aliyofanyiwa na redio ya Sauti ya Palestina kwamba, lengo jengine la safari hiyo ya Mahmoud Abbas huko New York Marekani ni kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani jinai za Israel za kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuendelea kuteka ardhi za Wapalestina.
Amesema, kwa mujibu wa Azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, uvamizi wa utawala wa Kizayuni na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.
Mwaka 2012, Palestina ilifanikiwa kuwa mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Mataifa baada ya wajumbe wengi wa Baraza Kuu la umoja huo kutambua rasmi uwepo wa nchi huru ya Palestina.
Tarehe 23 Disemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio ambalo lengo lake ni kukomesha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.
Lengo kuu la utawala wa Kizayuni wa Israel la kuteka ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii wa ardhi za Palestina na kuzipa sura ya Kizayuni ardhi hizo.