Russia: Magaidi karibu laki moja wameuawa Syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa, makumi ya maelfu ya magaidi wameuawa katika operesheni zilizofanywa na jeshi la nchi hiyo nchini Syria.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa, zaidi ya magaidi elfu 87 wameuawa katika mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya Syria na kwamba 830 miongoni mwao walikuwa vinara na viongozi wa makundi hayo.
Operesheni na mashambulizi hayo pia yameharibu vituo zaidi ya elfu moja vya makundi ya kigaidi na kuteketeza maghala karibu elfu kumi ya silaha na nishati ya magaidi hao.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, vifaru 650 na zaidi ya magari 700 ya kivita ya magaidi wa Syria waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na baadhi ya nchi kama Marekani na Saudi Arabia yameharibiwa.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya magaidi waliokuwa wakisaidiwa na nchi za kigeni kuvamia ardhi ya nchi hiyo kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo na kubadili mlingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa mslahi ya utawala haramu wa Israel. Juhudi hizo zimegonga mwamba na hatimaye Rais Donald Trump wa Marekani ameanza kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo nchini Syria huku nchi za Kiarabu zilizokuwa zimekata uhusiano na serikali ya Damascus zikishindana kurejesha tena uhusiano na mabalozi wao nchini Syria.