Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kuachiwa huru Nabeel Rajab
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50658-sisitizo_la_umoja_wa_mataifa_la_kuachiwa_huru_nabeel_rajab
Farhan Haq msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani namna utawala wa Aal Khalifa unavyokiuka uhuru wa kiraia huko Bahrain na kutaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Nabeel Rajab Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 05, 2019 09:25 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kuachiwa huru Nabeel Rajab

Farhan Haq msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani namna utawala wa Aal Khalifa unavyokiuka uhuru wa kiraia huko Bahrain na kutaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Nabeel Rajab Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha nchini humo.

Farhan Haq amesisitiza kuwa kuwekwa kizuizini Nabeel Rajab ni kinyume cha sheria. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa viongozi wa Bahrain inapasa watambue haki za raia wa nchi hiyo kuhusiana na "uhuru wa kutoa maoni". Utawala wa Aal Khalifa haujasita kuchukua kila aina ya hatua za kuwabana na kuwanyima wananchi wa Bahrain haki zao za msingi kabisa za kisiasa, kijamii na kiraia; na kueneza hali ya hofu nchini humo.

Farhan Haq, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN 
 

Katika mazingira kama hayo, wanaharakati wa kisiasa na wa haki za binadamu akiwemo Nabeel Rajab wamekuwa walengwa wa hatua hizo za kimabavu za utawala wa Aal Khalifa. Mahakama ya kimaonyesho ya utawala wa Aal Khalifa imemhukumu Nabeel Rajab kifungo cha miaka mitano jela. Askari usalama wa utawala huo tarehe 13 Juni mwaka 2016 walimtia mbaroni Nabeel Rajab akiwa nyumbani kwake. Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu yuko jela kuanzia wakati huo hadi sasa. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa polisi wa utawala wa Aal Khalifa wangali wanaendelea kutumia njia na mbinu zilezile kandamizi katika kuamiliana na wanaharakati wa kisiasa na wa haki za binadamu wa nchini Bahrain; huku wapinzani wakiendelea kufungwa jela na kuwekwa korokoroni kiholela kwa visingizio visivyo na msingi. Katika miaka ya karibuni walimwengu wameshuhudia rekodi nyeusi zaidi ya utendaji wa utawala wa Aal Khalifa kuhusu haki za binadamu kutokana na kushtadi jinai za utawala huo dhidi ya wananchi. 

Tovuti ya gazeti la L'Orient Le Jour (Lorien Le Jor) imetoa ripoti ikiutaja mwaka ulioisha wa 2018 kuwa mwaka mweusi na wa giza kwa watetezi wa haki za binadamu katika nchi za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi. Ripoti hiyo imeongeza kuwa: "Kuanzia Bahrain, Misri hadi Umoja wa Falme za Kiarabu, wanaharakati wa haki za binadamu wamepita kwenye kipindi ngumu sana katika mwaka uliopita wa 2018, khususan katika siku za mwisho za kumalizika mwaka ambapo tumeshuhudia hukumu za vifungo vikubwa jela zilizotolewa dhidi ya watetezi wa haki za binadamu katika nchi za Kiarabu. Kati ya nchi hizo za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi tunaweza kuashiria Saudi Arabia, Bahrain na Imarati." Ripoti hiyo imeashiria moja kwa moja hali ya Nabeel Rajab.  

Matokeo ya siasa zinazotekelezwa na utawala wa Aal Khalifa za kuwafunga jela idadi kubwa ya wamiliki wa vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za binadamu na wa kisiasa wa nchini Bahrain yamekuwa ni kuongezeka idadi ya wafungwa wa kisiasa katika jela za nchi hiyo. Imetangazwa kuwa Bahrain ina wafungwa wa kisiasa wasiopungua elfu tano, huku baadhi ya takwimu zikisema kuwa idadi ya wafungwa hao inafika elfu kumi. Kiwango hicho cha wafungwa wa kisiasa huko Bahrain kimeifanya nchi hiyo itambulike kama nchi yenye idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa duniani kwa kuzingatia idadi ndogo ya watu wa nchi hiyo. 

Siasa hizo zilizo dhidi ya ubinadamu za utawala wa Aal Khalifa za kukandamiza haki za raia zimeifanya Bahrain itambulike kama moja ya wakiukaji wakuu wa haki za binadamu katika uga wa kimataifa. Ripoti na misimamo ya viongozi wa Umoja wa Mataifa na ukosoaji mkubwa wa vyombvo vya kisheria kuhusu hatua hizo za utawala wa Aal Khalifa zinaonyesha kuwa Bahrain leo hii ni tatizo kuu katika uwanja wa  masuala ya kisheria. Katika hali ambayo walimwengu mwaka uliopita walitaraji kuwa jamii ya kimataifa itachukua hatua madhubuti kukabiliana na utawala wa Aal Khalifa kutokana na ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu, lakini bila ya kutazamia zilisikika taarifa kwamba nchi hiyo imepata uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa; hatua ambayo ni sawa na kuupa baraka kamili utawala huo ushadidishe jinai zake. 

Miamala yenye kugongana ya Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na tawala zinazokiuka haki za binadamu za Aal Khalifa na Aal Saud, ambapo kwa upande mmoja, umoja huo unatoa kauli za kuzikosoa tawala hizo, na kwa kwa upande mwingine unazipatia nafasi katika taasisi yake ya juu kabisa ya haki za binadamu, haijawa na matokeo mengine isipokuwa kuwafanya watawala wa nchi hizo za Kiarabu wawe na jeuri na uthubutu mkubwa zaidi wa kushadidisha jinai zao dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na wa vyombo vya habari katika nchi hizo. Kuuliwa kikatili Jamal Khashoggi mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud na kufungwa jela Nabeel Rajab mwanaharakati wa haki za binadamu mashuhuri wa nchini Bahrain ni natija ya miamala ya aina hiyo ya UN. 

Jamal Khashoggi, mwandishi habari aliyeuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki