Ansarullah ya Yemen: Tunaheshimu mazungumzo ya Stockholm
Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa harakati ya Ansarullah ya nchini humo inaheshimu na kutekeleza makubaliano ya kusitisha uhasama na mapigano yaliyofikiwa huko Stockholm nchini Sweden.
Hisham Sharaf amefanya mazungumzo mjini Sana'aa Yemen na Martin Griffiths Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na kuituhumu serikali ya Abdu Rabbuh Mansour Hadi rais aliyejiuzulu wa Yemen kuwa haiheshimu maamuzi ya mazungumzo ya Sweden. Ameongeza kuwa serikali ya Mansour Hadi inatumia baadhi ya vyombo vya habari kwa ajili ya kutangaza habari za uwongo.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen Jumamosi wiki hii aliwasili Sana'a kwa ajili ya kufuatilia na kufanya mazungumzo kuhusu namna ya kutekeleza makubaliano hayo ya kusitisha mapigano katika mji wa kistratejiai wa al Hudaydah.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyotiwa saini Stockholm nchini Sweden tarehe Sita Disemba mwaka jana, usitishaji vita ulipaswa kuanza kutekelekezwa tarehe 18 mwezi Disemba katika mji huo wa bandari. Hata hivyo muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia unaendelea kukiuka makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano. Umoja wa Mataifa tarehe 29 mwezi Disemba mwaka jana ulithibitisha katika taarifa yake kwamba, wapiganaji wa Ansarullah na jeshi la Yemen tayari wameondoka katika mji wa al Hudaydah.