Israel yanyunyizia kemikali za sumu katika mashamba ya Wapalestina wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50807-israel_yanyunyizia_kemikali_za_sumu_katika_mashamba_ya_wapalestina_wa_gaza
Katika kile kinachoonekana ni kushadidisha ukatili dhidi ya Wapalestina, utawala wa Kizayuni wa Israel umeripotiwa kunyunyizia kemikali za sumu katika mashamba ya kilimo ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2019 23:24 UTC
  • Israel yanyunyizia kemikali za sumu katika mashamba ya Wapalestina wa Gaza

Katika kile kinachoonekana ni kushadidisha ukatili dhidi ya Wapalestina, utawala wa Kizayuni wa Israel umeripotiwa kunyunyizia kemikali za sumu katika mashamba ya kilimo ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Wakulima wa Gaza waliohojiwa na shirika la habari la Russia Today wameitaja hatua hiyo ya Wazayuni kama 'sera ya vita vya kilimo'. Baadhi ya wakulima hao wa Kipalestina wamepuuzilia mbali madai ya utawala huo haramu, kwamba kemikali hizo husukumwa na upepo kutoka katika mashamba ya Israel na kuingia katika mashamba ya Wapalestina wa Gaza.

Wamesema mwezi uliopita wa Disemba, utawala huo wa kidhalimu bila ridhaa yao ulinyunyizia mashamba yao kemikali za sumu, kama vile glyphosate, ambayo imepigwa marufuku katika nchi nyingi duniani, kutokana na sumu yake hatarishi yenye kusababisha ugonjwa wa saratani.

Ahmed Badawi, mmoja wa wakulima hao wa Kipalestina ameiambia Russia Today kwamba, "Mimea katika shamba langu imeharibiwa kikamilifu na kemikali hizo, hatujui cha kufanya, jambo hili limekuwa likifanyika miaka nenda miaka rudi."

Sehemu ya athari za kemikali za sumu katika mashamba ya Wapalestina wa Gaza

Utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya himaya ya Marekani, umepuuza matakwa ya walimwengu ya kukomesha dhulma na mzingiro wa kibaguzi wa miaka 12 dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Itakumbukwa kuwa, kuanzia mwaka 2007 hadi hivi sasa, utawala wa Kizayuni umeshadidisha mashinikizo yake dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuufungia njia zote za kuingia na kutoka Ukanda wa Gaza ili kuwalazimisha wakazi wa ukanda huo waachane na muqawama na waipigie magoti Israel.