Kuongezeka safari za kidiplomasia nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50883-kuongezeka_safari_za_kidiplomasia_nchini_iraq
Jumbe tatu za kidiplomasia za Iran, Ufaransa na Jordan zimewasili nchini Iraq na kufanya mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 15, 2019 07:18 UTC
  • Kuongezeka safari za kidiplomasia nchini Iraq

Jumbe tatu za kidiplomasia za Iran, Ufaransa na Jordan zimewasili nchini Iraq na kufanya mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif amewasili Baghdad akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran na inasemekana kuwa, safari hiyo itaendelea mpaka siku ya Alkhamisi ijayo. Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian pia waliwasili jana mjini Baghdad. 

Safari za Zarif, Mfalme Abdullah wa Pili na Jean-Yves Le Drian nchini Iraq zinaweza kuchunguzwa katika pande kadhaa. Uhusiano wa Iran na Iraq ni miongoni mwa mahusiano ya kistratijia baina ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo katika safari yake ya sasa nchini Iraq, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran mbali na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Baghdad, vilevile amekutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa mashuhuri na viongozi wa kidini. Katika mkondo huo Zarif amesema katika mazungumzo yake na mwenyeji wake wa Iraq, Muhammad Ali al Hakiim kwamba: "Iran na Iraq zina historia inayofanana na uhusiano mkubwa na wa karibu baina ya watu wa mataifa haya mawili, na kila mwaka watu wa Iraq wanawakaribisha mamilioni ya wenzao wa Iran, hivyo hivyo watu wa Iran wanawapokea mamilioni ya ndugu zao wa Iraq; uhusiano huu ni imara sana kiasi kwamba, hauwezi kuingiliwa na upande wowote mwingine."

Zarif akihutubia mkutano wa kibiashara nchini Iraq.

Uhusiano wa Iraq na Jordan pia umo katika hali ya kustawi na kuimarika. Mwezi Novemba mwaka uliomalizika majuzi wa 2018 Rais Barham Salih wa Iraq alitembelea Jordan na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Tarehe 28 mwezi uliopita wa Disemba pia Waziri Mkuu wa Jordan, Umar al Razzaz alitembelea Baghdad. Hivyo, safari ya sasa ya Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan nchini Iraq inahesabiwa kuwa ni jibu kwa safari iliyofanywa na Rais Barham Salih nchini Jordan mwezi Novemba. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Mfalme wa Jordan ndiye kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu wa nchi ya Kiarabu kutembelea Baghdad tangu ilipoundwa serikali mpya ya Iraq Oktoba mwaka jana. Ajenda ya mazungumzo ya viongozi wa pande hizo mbili ni kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na kiusalama.

Safari za Mfalme wa Jordan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa nchini Iraq pia zinaweza kutathminiwa katika mtazamo mwingine tofauti. Jordan inaiangalia Iraq kama nchi yenye utambulisho wa Kiarabu na kwa msingi huo, serikali ya Aman na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zinafanya mikakati ya kuingilia masuala ya ndani ya Iraq na kujaribu kuvuruga uhusiano wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutumia karata ya "Uarabu".

Safari ya Mfalme wa Jordan nchini Iraq inafanyika siku moja tu baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian mjini Aman. Jana Jumatatu pia Le Drian mwenyewe aliwasili mjini Baghdad. Safari hizi zinafanyika sambamba na ile inayofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo  katika nchi za Kirabu za Mashariki ya Kati.

Pompeo akizungumza na Bin Salman, Saudi Arabia.

Japokuwa haionekani kwamba, lengo kuu la safari za sasa za maafisa wa nchi za Magharibi na za Kiarabu mjini Baghdad ni kujadili suala la kuundwa "Nato ya Kiarabu" dhidi ya Iran linalopigiwa debe na kutiliwa mkazo na Pompeo katika safari yake ya sasa kwenye nchi za Kiarabu, lakini ishara zote zinaonesha kwamba, miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa katika safari hizo ni jitihada za kuvuruga au kuharibu uhusiano wa Baghdad na Tehran na mgororo baina ya Palestina na utawala ghasibu wa Israel.