Tahadharisho la UNICEF kuhusu mauaji mapya ya watoto nchini Yemen
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto ulisema siku ya Jumatano kwamba, watoto elfu sita na 700 wa Yemen wameshauawa tangu Saudi Arabia na kundi lake walipoanzisha mashambulizi ya kila upande nchini humo.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeitaka Saudia na kundi lake zisimamishe mashambulizi mara moja huko nchini Yemen ili kuokoa watoto wa nchi hiyo wanaozidi kuteseka. Huku hayo yakisisitizwa na UNICEF, mashirikika mengine 14 ya kimataifa nayo yamekutana mjini London Uingereza kuzungumzia hali mbaya ya kibinadamu waliyo nayo hivi sasa wananchi wa Yemen. Kimberly Brown, Mkuu wa Sera za Misaada ya Kibinadamu wa Shirika la Msalaba Mwekundu ameyataka mataifa ya dunia kuwazingatiwa zaidi wananchi wa Yemen. Amesema: Watoto 85 elfu wa Yemen wamepoteza maisha yao kutokana na vita na madhara yake makubwa ikiwa ni pamoja na lishe duni. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 ya Umoja wa Mataifa, Yemen ndiyo nchi iliyokumbwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani.
Ukoo wa Aal Saud wa nchini Saudi Arabia chini ya mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Mohammad bin Salman, ulianzisha vita vya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya Magharibi. Kundi hilo la wavamizi wa Yemen limeizingira nchi hiyo ya Kiislamu kutokea angani, ardhi na baharini na linashambulia kila linachokiona bila ya kujali mashule, mahospitali, maghala ya vyakula, mabasi ya wanafunzi, miundombinu na chochote kingine. Hii ni katika hali ambayo muungano huo unaoongozwa na Saudia unaendelea kukwamisha juhudi zote za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen kama vile makubaliano ya kusimamisha vita katika mji wa bandari wa al Hudaydah yaliyofikiwa nchini Sweden. Ndege za kivita ambazo Saudi Arabia imepewa na madola ya kibeberu ya Magharibi zinaendelea kufanya mashambulizi ya kikatili nchini Yemen hasa katika mji mkuu San'a na kuwaua kikatili mamia ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa mujibu wa makubaliano ya nchini Sweden yaliyofikiwa tarehe 6 Disemba 2018, ilibidi usimamishaji vita uanze kutekelezwa tarehe 18 Disemba 2018 katika mji wa al Hudaydah, lakini muungano vamizi wa Saudi Arabia na mamluki wake umedharau makubalinao hayo na unaendelea kufanya jinai dhidi ya wakazi wa mji huo wakiwemo wanawake na watoto wadogo.
Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba jinai za mtawalia zinazofanywa na muungano vamizi wa Saudia huko Yemen zina baraka kamili za Marekani na udhaifu wa Umoja wa Mataifa. Misimamo ya kichochole sana inayochukuliwa na Umoja wa Mataifa imeifanya Saudi Arabia iendelea kufanya jinai dhidi ya watoto na raia wa Yemen bila ya woga wala wasiwasi wowote. Hadi hivi sasa mashirika ya umoja huo kama vile Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa yameshindwa kufanya lolote la maana kuwaokoa wananchi wasio na hatia wa Yemen mbele ya mashambulizi ya kinyama ya wavamizi wa nchi hiyo wanaoongozwa na Saudi Arabia na yanaishia kusema tu yanasikitishwa na maafa ya wananchi hao. Kama tulivyosema, Marekani inahusika moja kwa moja katika mateso wanayoyapata wananchi Waislamu wa Yemen. Nchi hiyo ya kibeberu inaipa misaada ya kila namna Saudi Arabia ikiwemo ya kijeshi, kisiasa, kilojistiki na hata taarifa za kijasusi ili iendelee kufanya mauaji nchini Yemen na hivyo Washington kuchangia pakubwa mgogoro wa kibinadamu nchini humo.

Kama tulivyotangulia kusema, Saudi Arabia inafanya mashambulizi ya kiholela bila ya kujali itasababisha madhara kiasi gani kwa raia wa Yemen. Kwa mfano jinai ya Saudi Arabia ya kushambulia mfumo wa kusafisha maji taka wa Yemen imepelekea kuzuka magonjwa hatari yakiwemo ya kipindupindu. Hayo yamethibitishwa na Senator wa Marekani, Bernie Sanders ambaye pia amesema: Vita nchini Yemen lazima visimamishwe na kuna wajibu wa kuwatumia misaada ya kibinadamu wananchi wa nchi hiyo na sio kuwashambulia kwa mabomu. Haifai kabisa kwa Marekani kuunga mkono umwagaji wa damu unaofanywa na Saudi Arabia nchini Yemen.
Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa, watu wenye hisia za kibinadamu hawafurahishwi hata kidogo na jinai zinazofanywa na Marekani na Saudi Arabia na kundi lao huko Yemen. Wajibu wa kukomesha maafa ya wananchi wa Yemen ni jukumu la kila mtu mwenye hisia za kibinadamu. Jukumu hilo linapaswa kutekelezwa hivi sasa, kwani wavamizi wa Yemen hawajali chochote, na ni miaka minne sasa wanaendelea kufanya jinai nchini humo bila ya hata kusutwa na nafsi zao.