Iraq: Hatutaruhusu ardhi yetu itumike kuihujumu nchi yeyote ile
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51365-iraq_hatutaruhusu_ardhi_yetu_itumike_kuihujumu_nchi_yeyote_ile
Waziri Mkuu wa Iraq amekosoa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump aliyedai kuwa wanajeshi wa Marekani wataendelea kuwepo nchini Iraq kwa shabaha ya kuipiga darubini Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 06, 2019 07:07 UTC
  • Iraq: Hatutaruhusu ardhi yetu itumike kuihujumu nchi yeyote ile

Waziri Mkuu wa Iraq amekosoa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump aliyedai kuwa wanajeshi wa Marekani wataendelea kuwepo nchini Iraq kwa shabaha ya kuipiga darubini Iran.

Adil Abdul-Mahdi aliyasema hayo jana Jumanne na kusisitiza kuwa, hakuna kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq, lakini kuna askari wa kutoa mafunzo wa US nchini humo, chini ya fremu ya muungano wa kimataifa, na kwamba Iraq haitakubali kutumiwa na nchi yeyote ile kwa ajili ya kuivamia au kuihujumu nchi nyingine.

Siaku ya Jumatatu Rais Barham Salih wa Iraq alisema katiba ya nchi hiyo hairuhusu kutumiwa ardhi ya Iraq kwa ajili ya kuishambulia nchi jirani na kwamba Trump hajaiomba idhini serikali ya Baghdad ya kutaka kuruhusiwa wanajeshi wa Marekani walioko nchini humo kuifuatilia Iran.

Matamshi ya Trump aliyoyatoa Jumapili iliyopita katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBS kwamba kuna umuhimu kwa Marekani kuendelea kuwa na kambi za kijeshi nchini Iraq kwa lengo la kuipiga jicho la karibu Iran, yameendelea kukosolowa katika pembe mbalimbali za dunia.  

Trump na mkewe walipowatembelea wanajeshi wa Marekani nchini Iraq hivi karibuni

Rais Hassan Rouhani wa Iran hapo jana alikosoa vikali kauli hiyo ya kiuhasama ya Trump, na kubainisha kuwa, "Mnatumia lugha ya porojo, isiyo ya kidiplomasia na isiyokubalika. Mnasema mtasalia Iraq ili kuipiga darubini Iran, katika hali ambayo awali mlidai mko katika nchi hiyo eti kupambana na ugaidi."

Amesisitiza kuwa, Wairani, Wairaqi na mtu yeyote yule duniani hawezi kuunga mkono msimamo na fikra hiyo ya Trump.