Ayatullah Sistani: Iraq haipasi kuwa kituo cha kuzidhuru nchi nyingine
-
Ayatullah Ali Sistani
Kiongozi mkuu wa kidini nchini Iraq Ayatullah Ali Sistani amesisitiza kuwa Iraq haipasi kuwa kituo kinachotumiwa kwa ajili ya kuzidhuru nchi nyinginezo.
Marjaa huyo mtajika wa Iraq amesema hayo siku kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutoa matamshi yanayoweka wazi sera za nchi hiyo za kuingiliaji kati masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Akizungumza leo na bi Jeanine Hennis Plasschaert, Mjumbe mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Misaada ya Umoja wa Mataifa huko Iraq (UNAMI), Ayatullah Sistani amesema kuwa: Iraq inataka kuwa na uhusiano mzuri, wenye mlingano na uliojengeka kwa msingi wa amani na maslahi ya pamoja na nchi zote jirani na bila ya uingiliaji kati wala kukiukwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.
Kiongozi huyo mkubwa wa kidini amesisitiza kuwa Iraq haipasi kutumika kama kituo cha kusababisha madhara na maafa kwa nchi nyingine.
Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Washington inaifuatilia Iran na eneo zima la Mashariki ya Kati kupitia kituo chake cha kijeshi kilichopo huko Ain al Asad mkoani al Anbar nchini Iraq.
Baada ya Trump kutoa matamshi hayo, Rais Barham Saleh wa Iraq, Waziri Mkuu Adil al Mahdi na Spika wa Bunge la nchi hiyo Mohamed al-Halbous walirudisha mapigo haraka wakisema kuwa kitendo cha kutumia ardhi ya Iraq dhidi ya nchi jirani ni kinyume cha katiba na mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo.