Palestina yasema haitashiriki mkutano wa Marekani wa Warsaw
Palestina imesema licha ya kupokea mwaliko, lakini haitahudhuria mkutano wa hapo tarehe 13 na 14 mwezi huu wa Februari huko Warsaw mji mkuu wa Poland, uliopewa anwani ya "Mkutano wa Amani na Usalama katika Mashariki ya Kati".
Katika ujumbe alioutuma jana Ijumaa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Saeb Erakat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema kuwa, "Msimamo wetu uko wazi, hatutashiriki kongamano hilo, na wala hatujamtuma mtu yeyote kwenda kuzungumza kwa niaba ya Palestina."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina kwa upande wake imeutaja mkutano huo wa Warsaw kama njama za Marekani za kutaka kuwashawishi watakaoshiriki kuidhinisha sera na mitazamo ya Washington kuhusu eneo la Mashariki ya Kati, haswa kadhia ya Palestina.
Mwezi uliopita pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitangaza kuwa, Moscow haitashiriki katika mkutano huo ulio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikisisitiza kuwa utafanyika katika fremu ya malengo ya Washinton inayoyafuatilia katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kadhalika Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amethibitisha kuwa, hatashiriki katika mkutano huo wa Marekani dhidi ya Iran uliopewa jina la "Mustakbali wa Mashariki ya Kati".
Baada ya nchi kadhaa kusema kuwa hazitashiriki mkutano huo, serikali ya Washington ilibadili kaulimbiu ya kikao hicho cha Warsaw kutoka 'Mkutano dhidi ya Iran' na kuwa mkutano kuhusu eneo la Mashariki ya Kati, ambao moja ya misingi yake mikuu ni kuasisi muungano wa kieneo kwa kuwashirikisha waitifaki wake wa Kiarabu na utawala haramu wa Israel, na kwa utaratibu huo kadhia ya Palestina iwekwe kando, na Iran na siasa zake katika eneo hili ziarifishwe kama tatizo kuu la Mashariki ya Kati.