Utawala katili wa Israel waendelea kumwaga damu za Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51432-utawala_katili_wa_israel_waendelea_kumwaga_damu_za_wapalestina_gaza
Vijana wawili wa Kipalestina wameuawa shahidi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika 'Maandamano ya Haki ya Kurejea' ambayo yalifanyika jana katika mpaka wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2019 04:17 UTC
  • Utawala katili wa Israel waendelea kumwaga damu za Wapalestina Gaza

Vijana wawili wa Kipalestina wameuawa shahidi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika 'Maandamano ya Haki ya Kurejea' ambayo yalifanyika jana katika mpaka wa Ukanda wa Gaza.

Ashraf al-Qidra, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Gaza amesema mmoja wa mabarobaro hao wa Kipalestina waliouawa shahidi ni kijana wa miaka 14 kwa jina Hassan Iyad Shalabi, aliyeuawa kwa kumiminiwa risasi kifuani katika mji wa Khan Yunis, yapata kilomita 25 kusini mwa Gaza.

Ameongeza kuwa, kijana mwingine mwanamapambano wa Kipalestina aliyeuawa shahidi jana anafahamika kama Mohammed Roshdi Ashtiwi, aliyekuwa na umri wa miaka 17, na ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi shingoni.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Gaza kadhalika amesema Wapalestina wengine 17 walioshiriki maandamano hayo ya jana wamejeruhiwa ima kwa risasi au mabomu ya kutoa machozi.

Askari Wazayuni wakiwalenga waandamanaji wa Kipalesina Gaza

Ukatili huo wa Israel umefanyika katika hali ambayo, Avigdor Lieberman, Waziri wa zamani wa Vita wa utawala haramu wa Israel ametoa wito wa kuanzishwa tena siasa za mauaji dhidi ya viongozi na wanamapambano wa Kipalestina huko katika Ukanda wa Gaza.

Wapalestina wasiopungua 250 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 26,000 wamejeruhiwa tangu yalipoanza 'Maandamano ya Haki ya Kurejea' katika mpaka wa Ukanda wa Gaza, mnamo Machi 30 mwaka jana.