Mtandao mkubwa wa kimataifa unaolifadhili kifedha DAESH Iraq wasambaratishwa
Shirika la Intelijensia la Iraq limeeleza katika taarifa maalumu iliyotolewa leo, kwamba limeugundua na kuusambaratisha "mtandao mkubwa zaidi wa ufadhili wa kifedha" kwa ugaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Shirika la Intelijensia la Iraq limeeleza kuwa, mtandao huo mkuu unajumuisha mitandao na matawi mbali mbali yaliyoko katika nchi tofauti duniani, ambayo kwa kutumia mbinu tata na za umahiri kupitia ofisi mbali mbali, yalikuwa yakichangisha na kukusanya fedha na kulipelekea kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH nchini humo.
Jana Jumatano, Shirika la Intelijensia la Iraq, lilitoa taarifa pia na kueleza kuwa, limewakamata wanachama wa mtandao mmoja uliokuwa ukiendesha harakati zake kwa kughushi vyeo vya baadhi ya maafisa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo, wakiwemo wa ofisi ya Waziri Mkuu na maafisa wa usalama na intelijensia.
Hivi karibuni, kufuatia kushamiri vitendo vya utekaji nyara na mauaji ya raia, ambayo yamekuwa yakifanywa na magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS), kiongozi wa mrengo wa Hikma ya Kitaifa ya Iraq, Ammar al Hakim, alivitaka vyombo vya usalama vifanye jitihada zaidi kuhakikisha wanaohusika na jinai hizo wanakamatwa na kushtakiwa.
Harakati za mabaki ya wafuasi waliotawanyika huku na kule wa kundi la Daesh zimeshadidi katika wiki za karibuni nchini Iraq, sambamba na kutolewa ripoti kadhaa za kuongezeka harakati za wanajeshi wa Marekani katika mikoa ya Nainawa, al Anbar, Salahuddin pamoja na maeneo mengine ya nchi hiyo yaliyokombolewa kutoka kwenye makucha ya kundi hilo la kitakfiri.../