Bahrain yawavua uraia makumi ya wanaharakati wa upinzani
Shirika huru la kutetea haki za binadamu limesema utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain umewafutia uraia makumi ya wanaharakati wa upinzani wa nchi hiyo katika kipindi cha wiki chache zilizopita.
Shirika hilo la Salam for Democracy and Human Rights lenye makao yake nchini Uingereza limeripoti kuwa, tangu mwezi uliopita wa Januari hadi sasa, utawala wa Aal Khalifa umewapokonya uraia wanaharakati 40 wa nchi hiyo.
Tovuti ya habari ya Bahrain Mirror imenukuu ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu na kuongeza kuwa, takwimu hizo mpya zimefanya idadi ya Wabahrain waliovuliwa uraia ndani ya nchi yao tangu mwaka 2012 hadi sasa ifikie 840.
Shirika hilo limesema kuwa, hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kufuta uraia wa idadi hiyo ya wananchi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na Manama inapaswa kuwarejeshea wananchi hao uraia wao.
Huku ukandamizaji ukiendelea nchini Bahrain, asasi mbalimbali za haki za binadamu zimekuwa zikitahadharisha kuhusu hali mbaya wanayokabiliwa nayo wafungwa katika magereza ya nchi hiyo.
Hivi karibuni shirika la Salam for Democracy and Human Rights lilitangaza kwamba, idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika jela kuu ya Bahrain, wamepatwa na maradhi mbalimbali kutokana na upuuzaji wa kuendelea unaofanywa na wakuu wa gereza hilo.