Wazayuni wawatia nguvuni wasimamizi wa Matukufu ya Kiislamu Quds
Polisi ya utawala haramu wa Israel imewakamata wasimamizi wa ngazi za juu wa Matukufu ya Kiislamu katika mji mtukufu wa Quds, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Miongoni mwa maafisa wakuu wa Quds waliokamatwa katika msako huo ulioanza usiku wa kuamkia leo ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wakfu wa Kidini, Sheikh Abdul Azim Salhab.
Mahdi Abdulhadi, mwanachama wa ngazi za juu wa wakfu huo amesema mbali na Sheikh Salhab na Naibu wake, maafisa wengine 13 wenye jukumu la kusimamia Matukufu ya Kiislamu huko Quds wametiwa mbaroni pia katika msako huo uliofanyika katika mji mtakatifu wa Baitul Muqaddas na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Jordan imetoa taarifa ikilaani kamatakamata na chokochoko hizo za polisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Makundi ya muqawama ya Palestina yanasisitiza kwamba, uchokozi na uvamizi huo wa utawala haramu wa Kizayuni unafanyika mbele ya kimya cha nchi za Kiarabu na Kiislamu, wakati huu ambapo baadhi ya watawala wa Kiarabu wako mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi.
Haya yanajiri huku hali katika msikiti wa al-Aqsa ikiwa tete na ya taharuki kufuatia hatua ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwafungia Waislamu Wapalestina Babu-Rahmah, moja ya milango ya kuingilia msikiti huo mtukufu.