Kumalizaka mazungumzo ya siku tatu ya Sheikhe mwanadiplomasia nchini Iraq
-
Rais Hassan Rouhani wa Iran ni maarufu kama Sheikhe mwanadiplomasia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatano alihitimisha mazungumzo yake na viongozi wa Iraq katika safari yake ya siku tatu nchini humo kwa kufika mji mtakatifu wa Najaf na kufanya mazungumzo na Ayatullah Sistani, marjaa taqlid wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Katika kikao hicho, Ayatullahil Udhma Sistani alikaribisha kuimarishwa kwa uhusiano baina ya Iraq na nchi jirani huku akizishukuru nchi rafiki kwa nafasi yao katika kuangamiza kundi la kigaidi la ISIS nchini humo.
Mkutano wa Rais Hassan Rouhani wa Iran na marjaa taqlid wa Mashia nchini Iraq una umuhimu mkubwa. Mkutano huo unaonyesha kuwa uhusiano wa Iran na Iraq kama nchi jirani umeimarika ambapo mbali na irada ya kisiasa ya nchi mbili, pia marjaa mkubwa zaidi wa kidini nchini Iraq ameunga mkono uhusiano huo.
Ayatullah Sistani ana nafasi ya kipekee katika jamii ya watu wa Iraq na alikuwa na nafasi kubwa sana katika vita dhidi ya magaidi wa ISIS nchini humo. Hatua ya marjaa huyo ya kuwataka wananchi kuungana na jeshi katika kukabiliana kwa pamoja na magaidi wakufurishaji wa ISIS, kulipelekea kuundwa kwa kundi la wananchi wapiganaji wa kujitolea maarufu kama Al Hashd Al Shaabi. Harakati hiyo ya wananchi iliweza kulisaidia jeshi kuangamiza magaidi wa ISIS nchini Iraq.
Hivyo ni wazi kuwa viongozi wa kidini nchini Iraq wana taathira chanya katika jamii ya nchi hiyo na ndio sababu mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ayatullah Sistani ukawa na umuhimu katika kuunga mkono uimarishwaji wa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya nchi mbili katika kipindi hiki cha baada ya kuangamizwa ISIS na kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.
Kutiwa saini mapatano matano ya ushirikiano baina ya Tehran na Baghdad katika safari ya Rais wa Iran nchini Iraq na kuondolewa malipo ya visa kwa wasafiri kutoka nchi mbili kuanzia mwezi ujao wa Aprili, na pia mapatano ya kujengwa miji ya kiviwanda katika mipaka ya pamoja na Iran na Iraq ni nukta zinazoashiria kuwa uhusiano wa nchi mbili ni wa kistratijia na hakuna upande wowote wa tatu unaoweza kuvuruga uhusiano huu.
Safari ya siku tatu ya rais wa Iran nchini Iraq na sisitizo la wakuu wa nchi mbili kuhusu kuimarisha uhusiano wa pande zote ni ujumbe wa wazi kuwa Iran na Iraq kama nchi mbili jirani zimechukua hatua imara za kuimarisha ushirikiano wao wa kistratijia.
Kuhusiana na hilo, Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumanne alijibu matamshi ya uingiliaji wa Brian Hook, mkuu wa "Kundi la Hatua Dhidi ya Iran' katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ambaye alionekana kutoridhishwa na safari ya rais wa Iran nchini Iraq. Katika jibu lake, Qassemi alimfahamisha Hook kuwa: "Iran na Iraq haziombi ruhusa kwa yeyote katika kuimarisha uhusiano wao."
Iran na Iraq kutokana na kuwa na nukta nyingi za pamoja za kiutamaduni, kilugha na kidini zinaweza kuimarisha uhusiano wao wa karibu katika kipindi hiki cha baada ya kuangamizwa ISIS nchini Iraq. Kama ambavyo Iran imekuwa pamoja na taifa la Iraq katika kipindi chote cha kupambana na magaidi wa ISIS, hivi sasa pia kama jirani mwenye kuaminika na mwenye kutegemewa, iko tayari kukidhi mahitaji mbali mbali ya Iraq.
Ushirikiano wa Iran na Iraq ni mfano wa uhusiano uliojengeka katika msingi wa ujirani mwema na kuheshimiana, na ushirikiano huu una mchango mkubwa katika kuleta usalama na amani katika eneo. Daima Iran imekuwa ikiunga mkono mchakato wa kisiasa na umoja wa makundi ya Iraq na katika fremu hii imeunga mkono kuundwa bunge la serikali mpya ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia uwazi wa sera za Iran kuhusu nchi jirani na nchi za eneo, na kwamba ushirikiano wa nchi za eneo ndio njia pekee ya kudhamini usalama, safari ya siku tatu ya rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iraq na mkutano wake na makundi mbali mbali ya Kishia, Kisunii, kikabila na marajii wa kidini nchini humo, ni dhihirisho la udiplomasia wa kuleta umoja unoafutiliwa na Iran katika eneo la kistratijia la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).