Makaburi tisa ya umati yagunduliwa katika mji wa Sinjar, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52245-makaburi_tisa_ya_umati_yagunduliwa_katika_mji_wa_sinjar_iraq
Mjumbe wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Iraq ametangaza taarifa ya kugunduliwa makaburi 9 ya umati ya raia wa Kiizadi waliouliwa na kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa Sinjar wa magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineveh) huko Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 18, 2019 11:02 UTC
  • Makaburi tisa ya umati yagunduliwa katika mji wa Sinjar, Iraq

Mjumbe wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Iraq ametangaza taarifa ya kugunduliwa makaburi 9 ya umati ya raia wa Kiizadi waliouliwa na kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa Sinjar wa magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineveh) huko Iraq.

Abdulwahid al Halfi amesema kuwa hadi kufikia sasa jumla ya makaburi 76 ya umati yameshagunduliwa huko Sinjar.

Kundi la kigaidi na la ukufurishaji la Daesh (ISIS) mwezi Juni mwaka 2014 liliivamia na kuteka sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq na katika siku za awali za uvamizi huo liliwauwa kwa umati watu wengi sana bila ya kujali itikadi zao za kidini na kimadhehebu, wakiwemo wanaume wa Kiizadi, watoto wa kiume na vibibi vikongwe zaidi ya 1,293 na kisha kuwazika katika makaburi ya umati. 

Raia wa Kiizadi wakiwalilia wapendwa wao waliouliwa na magaidi wa Daesh  
 

Al Halfi amezungumzia pia kuanza kufukuliwa moja ya makaburi hayo na kufanyiwa uchunguzi miili ya wahanga wa mauaji hayo ya kutisha. 

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana na baada ya kupita miaka minne ya uvamizi wa genge la kigaidi la Daesh, jumla ya watoto wa Kiizadi 3,083 wakiwemo mabinti 1,427 walikuwa bado wangali wanashikiliwa na kundi hilo la kigaidi.